CAF: Soka ya Afrika katika njiapanda | Michezo | DW | 04.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

CAF: Soka ya Afrika katika njiapanda

Shirikisho la soka barani Afrika CAF litachagua rais mpya mnamo Machi 12. Mkuu wake wa zamani Ahmad Ahmad amepigwa marufuku na FIFA, lakini bado anaweza kugombea. Je! taswira ya CAF iliyoharibiwa itaendelea kuteseka?

Je! ataendelea kupigwa marufuku au rais wa zamani wa CAF Ahmad Ahmad atagombea uongozi Machi 12? Swali hili siyo tu linaishughulisha kandanda ya Afrika, bali pia mahakama ya kimataifa ya utatuzi wa mizozo ya kimichezo, CAS.

Mwisho wa Januari CAS ilikubali kuongeza kasi ya mchakato wa kusikiliza rufaa iliyowasilishwa na Ahmad. Rais huyo wa zamani wa shirikisho la Soka Africa alipigwa marufuku kushika nyadhifa zote kwa miaka mitano na Kamati ya Maadili ya Fifa Novemba iliyopita.

Soma pia: CAF yashikilia uamuzi wake kuhusu Rwanda

Taarifa ilisema Ahmad alikwenda kinyume na jukumu lake la utiifu, alitoa zawadi na faida nyingine, alifanya ubadhirifu wa fedha na kutumia vibaya nafasi yake kama mkuu wa CAF. Hatua ya CAS kuidhinisha uharakishaji wa mchakato imewashangaza wengi.  Inamaanisha kuwa Ahmad anaweza kurudi kwenye kampeni wakati akisubiri CAS kuthibitisha uamuzi wake katika wiki ya kwanza ya Machi.

FIFA Gianni Infantino und Ahmad Ahmad

Rais wa FIFA Gianni Infantiono akiwa na Ahmad Ahmad mjini Casablanca, Februari 2, 2018.

Februari 6, Kamati ya Utendaji ya CAF, mjini Yaoundé, Kamerun, ilikuwa tayari imeamua kwamba FIFA italazimika kuamua ikiwa Ahmad anastahili kushiriki uchaguzi. Kwa upande mwingine, Tume ya Utawala ya CAF, haikuwa na pingamizi kwa rais huyo wa zamani kushiriki katika uchaguzi wa tarehe 12 Machi. Waangalizi wanachukulia kuwa FIFA haitamruhusu Ahmad kugombea nafasi hiyo bila kujali uamuzi utakaotolewa na Mahakama ya Michezo CAS.

Uchaguzi kutoka mwamko mpya

Mansour Loum mwanahabari wa michezo ambaye amekuwa akifuatilia soka kwa miaka kadhaa ameiambia DW kuwa Shirikisho la Soka Africa limedhoofika kama taasisi na imefikia ukingoni na uchaguzi mpya utatoa nafasi kwa mwamko mpya.

Bila kujali ikiwa Ahmad atashiriki katika uchaguzi huo, wagombea wengine wanne wa urais tayari wamejitokeza. Mmoja ni bilionea wa Afrika Kusini Patrice Motsepe ambaye ni shemeji wa Rais Cyril Ramaphosa na amepata utajiri mkubwa katika madini.

Soma pia: CAF kuamua kuhusu la Kombe la Mataifa Afrika

Kampuni yake ya madini iitwayo "African Rainbow Minerals" inajumuisha migodi ya makaa ya mawe, chuma, nikeli, shaba, dhahabu na platinam. Pia ni rais wa klabu ya soka ya daraja la kwanza Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns kutoka Pretoria. Motsepe ana ari ya kuwania nafasi hio lakini vyombo kadhaa vya habari vinadai kuwa shirikisho la soka Afrika Kusini halimpi ushirikiano.

Afrika Fußball Jacques Anouma

Jacques Anouma ni mgombea wa nafasi ya rais kutoka Ivory Coast.

Mgombea mwengine ni Jacques Anouma, mwenye umri wa miaka 70 ambaye ni rais wa Chama cha Soka cha Cote di'Voire. Ni maarufu kwasababu ameboresha viwango vya kitaaluma huko Cote d'Ivoire. Anouma amekuwa rais wa shirikisho hilo tangu 2002 na pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FIFA kutoka 2007 hadi 2015.

Mwandishi wa habari wa Cote di'voire Augustin Kouyo amesema Anouma anaungwa mkono kikamilifu Cote di'voire. Na serikali ya Ivory Coast imetuma wajumbe katika nchi zingine za Kiafrika ili kumpigia upato Anouma. Wagombea wengine wawili ni Ahmed Yahya na Augustin Senghor, wanaongoza vyama katika nchi zao, Mauritania na Senegal mtawalia.

Katika kinyanganyiro cha Machi 12, Wagombea Anouma, Yahya na Senghor wote wanatoka Afrika Magharibi, Shirikisho la Soka Africa halijawahi kuwa na rais kutoka eneo hilo.

Lakini, inatia shaka kama Yahya na Senghor watabaki kwenye kinyang'anyiro ikiwa Ahmad Ahmad pia atakubaliwa. Wote wawili walikuwa wameahidi kumuunga mkono Ahmad katika uchaguzi kabla ya kupigwa marufuku kwake.

Mwandishi wa habari wa Michezo Mansour Loum amesema uchaguzi huo ni muhimu sana kwa  atakayeshinda mnamo Machi 12 na kwa sababu kwa mara ya kwanza kuna wagombea wengi pia mshindi atakua na jukumu la kujaribu kurudisha taswira nzuri ya taasisi hio ya michezo ambayo imepoteza heshima na ushawishi kutokana na mapambano mengi ya ndani ya FIFA.