Burkina Faso na Misri kupambana nusu fainali AFCON | Michezo | DW | 01.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Burkina Faso na Misri kupambana nusu fainali AFCON

Mashindano ya kandanda ya Kombe la mataifa ya Afrika, fainali zinazofanyika nchini Gabon, yanaingia hatua ya nusu fainali ambapo Jumatano usiku Burkina Faso itamenyana na miamba ya kaskazini Misri mjini Libreville.

Timu ya taifa ya soka Misri ikifanya mazoezi

Timu ya taifa ya Misri ikifanya mazoezi

Burkina Faso ilifanikiwa kutinga nusu fainali kwa  kuibwaga Tunisia mabao 2-0 na Misri ikamfunga hasimu yake Morocco bao1-0. Mchezaji wa  nafasi ya ulinzi wa Burkina faso Bakary Kone  anayecheza katika kilabu ya Malaga katika  ligi  kuu ya uhispania  La liga amesema wana matumaini makubwa ya kucheza fainali, huku  Kocha wa Burkina Faso Mreno Paulo Duarte naye akisisitiza kwamba lengo lao ni  kuiangusha Misri  leo na kufika fainali . Burkina Faso itakuwa ikisaka  nafasi nyengine ya kucheza fainali baada ya ile fainali ya 2013. Timu hizi zilikwisha kumtana katika nusu fainali miaka 21 iliopita pale Misri ilipoifunga  Burkina Faso na  hatimaye katika mechi ya fainali ikalitwaa kombe hilo la mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza. Kocha waburkina Faso Mreno Paulo Duarte amepokea  salamu za kumtaka  kila la kheri, kutoka  kwa mwananchi mwenzake Kocha wa Manchester United Jose Mourinho. Duarte amemulezea  Mourinho kuwa sio tu ni rafiki bali ni kama baba kwake.

Misri itakuwa tena uwanjani na mlinda mlango Essam el-Hadary  mwenye umri wa miaka 44  na aliyeshinda mataji yote manne ya  Kombe hilo  akiwa na Misri, ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni miaka 19 iliopita. Ni vigumu kutabiri matokeo ya pambano hilo la leo na Mwalimu wa Misri  Hector Cuper kutoka Argentina mwenye umri wa miaka 61 aliyewahi kuzifunza Valencia ya Uhispania na Inter Milan ya Italia, anasema  licha ya majeruhi, wachezaji wake wako imara kuwakabili wapinzani wao.

Cameroon kumenyana na Ghana

Timu tatu zilizofanikiwa kuandika historia katika mashindano ya kandanda ya kombe la mataifa ya Afrika- Misri, Ghana na Cameroon  zote  zinaingia katika nusu fainali ya mashiondano ya safari hii, kila moja ikiwa imeshanyakuwa ubingwa mara nne. Baada ya nusu fainali kati ya Burkina Faso na Misri mjini Libreville, Alhamisi mjini Franceville itakuwa ni zamu ya Cameroon kutoana jasho na Ghana. Cameroon itakuwa inatafuta nafasi ya  kumaliza kiu cha miaka 15 na Ghana ikiwania safari hii hatimaye kufuta machozi baada ya kulikaribia taji bila ya mafanikio kwa miaka 35.

Ghana itaingia uwanjani na kuuweka kando mkasa uliomkumba mlinda mlango wake Razak Brimah aliyetozwa faini ya dola 2,500 hapo jana kutokana na  video aliyoiweka kwenye ukurasa wake wa Facebook. Video hiyo iliwalenga  mashabiki waliomkosoa kwa baadhi ya matukio uwanjani. Razak aliwajibu kwa maneno haya "Ninyi na familia Zenu mnaweza kutokomea."  Mchezaji huyo baadae aliomba radhi.Kuingia nusu fainali hiyo kesho, Ghana iliiadhibu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mabao 2-1 na Cameroon ikaibwaga Senegal moja ya  timu zilizoekewa matumaini ya kufika fainali,  kwa uamuzi wa  matuta yaani  mikwaju penalty, baada ya dakika  120 kumalizika bila ya kufungana. Fainali ya mashindano hayo itachezwa Jumapili.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman

Mhariri: Iddi Ssessanga