Bunge nchini Kenya kukutana leo | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 06.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Bunge nchini Kenya kukutana leo

Kikao hicho kufungua njia ya kuidhinishwa hatua ya kugawana madaraka na kumaliza machafuko.

default

Mpatanishi Kofi Anna(katikati) akiwa na rais Mwai Kibaki (kushoto) na kulia ni kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Bunge la 10 nchini Kenya lilifunguliwa kwanza Januari 15 wakati machafuko ya kisiasa yalipokua yamepamba moto yakiandamana na mauaji ya kikabila ambapo watu karibu 1,500 walipoteza maisha .

Baada majuma kadhaa ya upatanishi ulioongozwa na Katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan, Rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani wa chama cha ODM Raila Odinga ambaye alidai alipokonywa ushindi katika uchaguzi wa rais, wakafikia makubaliano ya kugawana madaraka tarehe 28 mwezi uliopita.

Chama cha ODM cha Raila kilikiangusha chama cha PNU cha rais Kibaki katika uchaguzi wa bunge kikishinda wingi wa viti bungeni. Kutokana na mapatano yaliofikiwa, pande zote mbili zimeahidi kuunga mkono muswada wa sheria utakaowasilishwa bungeni juu ya kugawana madaraka.

Rais Kibaki leo anauongoza mkutano wa kundi la pamoja la wabunge juu ya serikali ya muungano na baadae alasiri atakifungua rasmi kikao caha bunge. Pande zote mbili zimekubaliana kuunda kamati itakayoandaa sera za serikali ya mseto itakayoundwa mnamo siku chache au majuma machache yajayo.

Raila Odinga anatarajiwa kuwa Waziri mkuu mpya, lakini kunatarajiwa pia kuwepo kwa hali ya vuta ni kuvute kuwania nyadhifa muhimu. Iwapo makubaliano yatafikiwa,serikali hiyo ya muungano inayotaarajiawa, itachukua nafasi ya ile iliotangazwa na rais Kibaki siku chache baada ya kuapishwa haraka haraka, mara tu alipotangazwa mshindi katika hali ya kutatanisha.


Machafuko yaliotokana na uchaguzi huo yameuathiri vibaya uchumi wa taifa hilo la Kenya na kufufua uhasama kuhusiana na masuala ya ardhi, umasikini na kile kinachoonekana kama ni mkakati wa baadhi ya wanasiasa kutoka kabila la Kikuyu kutaka kuendelea kuwa na mamlaka ya kisiasa na kibiashara nchini humo.

Wakati huo huo,serikali imekanusha vikali madai ya shirika la utangazaji la Uingereza BBC kwamba kulifanyika mikutano ya siri kati ya maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ya rais Kibaki na kundi la wanamgambo lililopigwa marufuku la MUNGIKI na lengo lilikua ni kuwaajiri wanamgambo hao kama kikosi cha kinga katika eneo la bunde la ufa (Rift Valley) kuilinda jamii ya wakikuyu.

Inasemekana mkutano huo ulifanyika nyumbani kwa rais Kibaki na ripoti imedai BBC iliarifiwa na mtu mmoja kutoka Kabila hilo la kikuyu akisema wao kama Mungiki walihusika katika machafuko hayo na kuwa wanachama watatu wa Mungiki walikutana Ikulu na maafisa wa serikali ya rais Kibaki.

Hata hivyo serikali imekanusha madai hayo huku msemaji wake Alfred Mutua akisisitiza kamwe hakujawahi kuweko na mikutano ya aina hiyo.

 • Tarehe 06.03.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DJK6
 • Tarehe 06.03.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DJK6
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com