1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Bunge la Scotland lamthibitisha Yousaf kuwa Waziri kiongozi

28 Machi 2023

Bunge la Scotland limemthibitisha leo hii Humza Yousaf kama waziri kiongozi mpya baada ya kushinda kinyang'anyiro cha kumrithi Nicola Sturgeon kama kiongozi wa Chama cha Kitaifa cha Scotland (SNP).

https://p.dw.com/p/4POhT
Schottland Edinburgh | Schottlands Gesundheitsminister Humza Yousaf nach Wahl zum SNP-Parteivorsitzenden
Picha: Jeff J Mitchell/Getty Images

Yousaf aliwashinda siku ya Jumatatu wapinzani wake wawili katika chama cha SNP na kunyakua wadhifa wa juu wa chama hicho, akiahidi kufufua harakati zake za kupigania uhuru wa Scotland.

Akiwa na umri wa miaka 37, Yousaf amekuwa waziri kiongozi wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi tangu kufanyika mageuzi ya Bunge la Scotland kuhusu ugatuzi mnamo mwaka 1999, na kiongozi wa kwanza wa Kiislamu wa chama kikuu cha siasa nchini Uingereza. 

Katika hotuba yake ya ushindi, Yousaf amesema akiwaambia wanachama wa SNP kuwa wote wanapaswa kujivunia ukweli kwamba leo hii wametuma ujumbe uliowazi kwamba rangi ya ngozi au imani ya mtu sio kizuizi cha kuongoza nchi hiyo.

England Gesundheitsminister Yousaf wird neuer schottischer Regierungschef
Humza Yousaf aliyeshinda uchaguzi katika Chama cha SNP na aliyethibitishwa na Bunge kuwa waziri mkuu mpya wa ScotlandPicha: JANE BARLOW/AFP

Akiahidi kuwa kiongozi kwa wa raia wote wa Scotland, Yousaf ameahidi kuanzisha vuguvugu la kiraia ambalo amesema litahakikisha harakati zao za uhuru zikisonga mbele kwa hatua kubwa, na kusisitiza kuwa wao watakuwa kizazi kitakachoipatia Scotland uhuru wake.

Soma pia: Yousaf kuwa waziri kiongozi mpya wa Scotland

Wabunge wa Scotland wamemthibitisha waziri kiongozi mpya huyo ili kumrithi Nicola Sturgeon ambaye alijiuzulu.

Saa chache kabla ya kura hiyo, Sturgeon alituma barua rasmi ya kujiuzulu kwa Mfalme Charles III, na kuondoka katika makazi rasmi ya waziri mkuu huko Edinburgh.     

Mabadiliko katika siasa za Scotland

Schottland Edinburgh | Nicola Sturgeon, Regierungschefin | Bekanntgabe Rücktritt
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Scotland Nicola SturgeonPicha: Jane Barlow/REUTERS

Yousaf ataapishwa kama waziri kiongozi katika sherehe itakayofanyika siku ya Jumatano, baada ya uthibitisho rasmi kutoka kwa mfalme Charles III. Viongozi wa chama cha SNP wamejivunia kwamba Scotland imekuwa taifa la kwanza la kidemokrasia katika eneo la Ulaya Magharibi kumchagua Mwislamu kama kiongozi mkuu.

Mabadiliko hayo ya kushangaza katika siasa za Scotland yanafuatia tangazo la kushtukiza la kujiuzulu kwa Sturgeon mwezi uliopita baada ya kuongoza kwa zaidi ya miaka minane.

Soma pia: Kiongozi wa Scotland atangaza kujiuzulu

Msemaji wa waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amewaambia waandishi wa habari kwamba kiongozi huyo mpya wa SNP anapaswa kuzingatia masuala ya kiuchumi na sera muhimu kwa wapiga kura wa Scotland.

Yousaf, ambaye alikuwa waziri wa afya katika uongozi wa Sturgeon, alipata ushindi mfinyu katika kinyang'anyiro cha SNP kwa kujikusanyia asilimia 52 ya kura. Alikabiliwa pia na ukosoaji juu ya rekodi yake katika majukumu kadhaa serikalini.

Kwa sasa Humza Yousaf anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwavutia wapiga kura wengi zaidi wa Scotland, huku uchaguzi mkuu wa Uingereza ukitarajiwa kufanyika katika kipindi cha miezi 18 ijayo.