Bundesliga:Hamburg na Bayer Leverkusen kileleni. | Michezo | DW | 28.09.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bundesliga:Hamburg na Bayer Leverkusen kileleni.

Leverkusen yaitoa Cologne 1:0: Hamburg Munich 1:0

default

Lukas Podolski wa Cologne atiwa munda na Leverkusen.

-Katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani, timu 2 za kileleni zalitamba: Bayer Leverkusen yawika mjini Cologne kwa bao 1:0 na Hamburg yaizaba Bayern Munich bao 1:0.

-Katika Premier League-ligi ya Uingereza-

Chelsea imetimuliwa kileleni na Wigan Athletic.

-Afrika Kusini,miezi michache kabla Kombe la dunia, imejipatia rais mpya wa Shirikisho lake la dimba.

Bundesliga:Ligi ya Ujerumani:

Baada ya Jumamosi , timu 2 za kileleni, kuimarisha nafasi zao-Bayer Leverkusen kwa kuizaba FC Cologne nyumbani bao 1:0 na Hamburg ikitamba na mbrazil, Ze Roberto kuitimua Bayern munich pia kwa bao 1:0, jana ilikua zamu ya Hoffenheim na Freiburg kutamba:

Timu ya Hoffenheim iliozusha mshangao msimu uliopita, sasa inarudi upya kutia fora usoni. Hoffenheim jana ilirudi kutamba ilipoichezesha timu ya jiji kuu, Hertha Berlin, kindumbwe-ndumbwe na kuitandika mabao 5-1. Pigo hilo kali limezusha swali kwa muda gani zaidi kocha wa Berlin, mswisi Havre atabakia kocha wa timu hiyo.Wengi wanahisi siku zake zimehesabiwa. Binafsi, kuhusu pigo la jana, anasema:

"Hakuna anaeridhika katika hali kama hii. Na jambo hilo ni wazi kabisa. Lakini kwa mara nyengine tena , baada ya kushindwa huko wazi , nisingependa kusema zaidi."Hoffenhiem sasa inasimama nafasi ya 3 ya ngazi ya ligi.

Katika changamoto ya pili jana jioni, SC Freiburg ilitia mabao 3 katika kipindi cha pili cha mchezo na kutoroka na pointi 3 katika mpambano wake na Borussia Moenchengladbach. Sasa Freiburg, iliopanda msimu huu daraja ya kwanza imeangukia nafasi ya 10 ya ngazi ya Ligi.

Katika mapambano 2 ya kileleni, Hamburg ilizima vishindo vya mabingwa mara kadhaa, Bayern Munich, na kunyakua pointi 3 nyengine. Sasa Hamburg yaongoza Bundesliga kwa pointi 17 ikiipiku Bayer Leverkusen ilioilaza hasimu wake wa mtaani, FC Cologne, kwa bao 1:0 kwa wingi wa magoli tu.

Huko Uingereza, "aliejuu ,mgoje chini": Chelsea, ilizabwa mabao 3:1 na Wigan Athletic na kupoteza usukani wa kuongoza Premier League. Msukosuko uliwapata Chelsea pale kipa wao Peter Cech alipotimuliwa nje ya lango lake na rifu kwa kucheza ngware huku matokeo yakiwa bao 1:1.

Chelsea ilioshinda mapambano yake 6 yaliopita, sasa imeangukia nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi. Manchester United sasa imeshika uongozi kwa tofauti ya magoli tu na kufuatia ushindi wake jana wa mabao 2-0 huko Stoke City. Manu na Chelsea kila moja sasa ina pointi 18.Liverpool na Tottenham Hotspur zina pointi 15 kila moja.

Ama katika La Liga-Ligi ya Spain, Real Madrid na mahasimu wao wakubwa FC Barcelona waliendelea kushinda kwa mara ya 5 tangu kuanza msimu huu.

Barcelona ilinguruma huko Malaga pale Zlatan Ibrahimovic alipoendelea na rekodi yake ya kutia bao kila mchezo. Real imeitandika Tenerife mabao 3:0.Sevilla ikaikumta bilbao mabao 4-0 na sasa inanyatia kutoka nafasi ya 3 ya ngazi ya Ligi.

Katika Serie A,Ligi ya Itali, Sampdoria kwa mshangao wa mashabiki wake na maadui sasa ndio viongozi wa Ligi na sio Inter au AC Milan. Giampaolo Pazzini, alitoboa pazia la lango la Inter,mabingwa na kutia bao pekee la ushindi kwa Sampdoria.

Juventus wako sasa pointi 1 nyuma ya Genoa kwani, walizimwa sare bao 1-1 nyumbani na Bologna. Inter Milan sasa wako nafasi ya 3 bia pamoja na Fiorentina ambao wanajiwinda kwa changamoto ya kesho ya Champions league -kombe la klabu bingwa barani Ulaya kati yao na FC Liverpool ya Uingereza.

Kinyanganyiro cha kugombea uongozi wa Shirikisho la dimba la Afrika Kusini, SAFA, kimemalizika kwa ushindi wa Kirsten Nematandani. Mwenyekiti wa Kamati ya maandalio ya kombe la dunia Danny Jordaan na msaidizi wake Irvin Khoza walijitoa katika kinyanganyiro hicho cha kugombea urais wa SAFA.Nematandani alichaguliwa bila ya kupingwa.

Kulikuwapo malalamiko hapo kabla,kwamba kinyanganyiro hicho cha kugombea kiti cha Shirikisho la dimba la Afrika Kusini, kikiweka pingamizi katika maandalio ya Kombe lijalo la dunia Juni mwaka ujao.Ilisemekana endapo Jordaan au khoza angechaguliwa kuliongoza shirikisho hilo, basi asingeweza kukamilisha ipasavyo kazi za maandalio ya Kombe la dunia.

Muandishi: Ramadhan Ali / RTRE

Mhariri: O.Miraji

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com