1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Johnson kuchukua mikoba ya Theresa May

Amina Mjahid
24 Julai 2019

Boris Johnson anatazamiwa kuapishwa rasmi kama Waziri Mkuu wa Uingereza. Jonson pia anatarajiwa kutangaza majina ya kundi atakalolipa majukumu ya kuendesha mchakato wa kuiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/3MeVZ
Großbritannien London | Boris Johnson posiert vor dem Hauptquartiert der Konservativen
Picha: Getty Images/D. Kitwood

Boris Johnson ataanza kuiongoza Uingereza kuanzia hii leo mchana wakati Waziri Mkuu Theresa May atakapomkabidhi rasmi mkoba huo wa uongozi.

May alitangaza kujiuzulu mwezi uliyopita baada ya kushindwa kuwashawishi wabunge kuunga mkono mapendekezo yake ya kuiondoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya.

Boris anaingia katika ofisi ya Downing Street hii leo wakati Uingereza ikiwa imegawika juu ya suala la Brexit na kudhoofika kutokana na mgogoro huo wa kisiasa wa miaka mitatu tangu kura ya maoni ya kujiondoa katika Umoja huo ilipopigwa.

Großbritannien London | Theresa May verlässt Downing Street zum letzten mal als Premierministerin
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/J. J. Mitchell

Baada ya kumkabidhi Jonson madaraka, Bi May ataelekea moja kwa moja hadi katika ikulu ya Buckingham kukutana na Malkia Elizabeth ili amfahamishe rasmi juu ya kujiuzulu kwake.

Kisha Waziri Mkuu mpya baada ya kuapishwa Boris Johnson atakuwa pia na mazungumzo na Malkia Elizabeth na kutarajiwa kuwateua wanachama muhimu atakaofanya nao kazi katika serikali yake.

Majina hayo yanatarajiwa kutoa picha kamili ya namna atakavyolishughulikia suala la Brexit.

Ahadi aliyoitoa Johnson ni kuiondoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31 kwa makubaliano au bila makubaliano, hatua ambayo huenda ikaiingiza Uingereza katika mgogoro wa kikatiba au kufanyika kwa uchaguzi wa mapema.

"Tunakwenda kuipa nguvu nchi hii, tutaufanikisha mpango wa Brexit ifikapo Oktoba 31 na tutachukua fursa zote tutakazozipata kutokana na Brexit hii kwa nia ya tunaweza." alisema Jonson.

Waziri Mkuu mpya kuelezea mipango yake ya Brexit bungeni 25.07.2019

Hapo jana chama tawala cha Conservative nchini humo kilimchagua Boris Johnson kwa kishindo kuwa kiongozi wa chama hicho hatua iliyompa nafasi ya kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza na kufungua ukurasa mpya katika siasa za nchi hiyo.

Großbritannien London | Boris Johnson wird neuer Premierminister
Waziri Mkuu mtarajiwa wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Getty Images/AFP/T. Akmen

Johnson alimshinda mpinzani wake waziri wa masuala ya kieni wa sasa nchini humo Jeremy Hunt

Waziri Mkuu huyo mpya anatarajiwa kesho Alhamisi kutoa hotuba katika bunge la Uingereza kuelezea mipango yake juu ya Brexit.

Wakati huo huo, salamu zimezidi kumiminika kumpongeza Boris Johnson katika safari yake ya kuingoza Uingereza licha ya changamoto nyingi zinazomkabali. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alimpongeza kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ni miongoni pia mwa waliompongeza Johnson kwa uteuzi wake na kusema wanatarajia kufanya kazi naye vizuri huku Erdogan akisema mahusiano ya Uturuki na Uingereza yataimarika zaidi chini ya uongozi wa Johnson.

Vyanzo: dpa/Reuters/afp