1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bolivia yawafukuza mabalozi wa Uhispania, Mexico

Mohammed Khelef
31 Desemba 2019

Rais wa mpito wa Bolivia, Jeanine Anez, amesema serikali yake imeamua kuwafukuza mabalozi wa ngazi za juu wa Mexico na Uhispania na Uhispania nayo imewafukuza maafisa watatu wa ubalozi wa Bolivia kujibu hatua hiyo. 

https://p.dw.com/p/3VWcG
Bolivien Interimspräsidentin Jeanine Anez
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Karita

Rais wa mpito wa Bolivia, Jeanine Anez, amesema serikali yake imeamua kuwafukuza mabalozi wa ngazi za juu wa Mexico na Uhispania, baada ya jaribio la maafisa wa serikali ya zamani kuondoka kwenye ubalozi wa Mexico kwa msaada ya balozi wa Uhispania na kutoroka nchi. 

Rais Anez amesema kuwa Balozi Maria Teresa Mercado wa Uhispania na afisa wa ubalozi huyo anayehusika na usalama hawatakiwi kuwapo Bolivia ndani ya masaa 72 yajayo. 

Uhispania nayo imewafukuza maafisa watatu wa ubalozi wa Bolivia kujibu hatua hiyo. 

Mkasa huu unawahusu maafisa tisa wa serikali ya Rais Evo Morales iliyopinduliwa kufuatia maandamano ya umma na uingiliaji kati kijeshi, ambao waliomba hifadhi kwenye ubalozi wa Mexico.

Serikali ya mpito ya Bolivia imewafungulia mashitaka maafisa hao wakiwatuhumu kwa uchochezi, ugaidi na wizi wa kura, na imewakatalia kutoka nje ya nchi.