Boko Haram wapanga kuzishambulia balozi za Marekani, Uingereza | Matukio ya Afrika | DW | 12.04.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

VITA DHIDI YA BOKO HARAM

Boko Haram wapanga kuzishambulia balozi za Marekani, Uingereza

Nigeria imewakamata wapiganaji kadhaa wa Boko Haram kwa kupanga mashambulizi dhidi ya balozi za Marekani na Uingereza, huku idadi ya watoto wanaotumika kwenye mashambulizi ya kundi hilo ikiongezeka. 

Idara ya Usalama ya Nigeria (DSS) inasema inawashikilia wapiganaji wa tano wa Boko Haram ambao wana mafungamano na kundi la Dola la Kiislamu (IS) katika jimbo la Benu na kwenye mji mkuu, Abuja. 

Kwa mujibu wa msemaji wa Idara hiyo, Tony Opuiyo, watuhumiwa hao walikuwa wamekamilisha mipango ya kuzishambulia balozi hizo na maeneo mengine yenye maslahi na mataifa ya Magharibi. "Tunaendelea na uchunguzi zaidi," aliongezea msemaji huyo bila kutaja undani wa kile walichokigundua.

Kundi la Boko Haram limekuwa tishio kubwa kwenye jamii za kaskazini mashariki mwa Nigeria, ambako linasema linataka kuanzisha utawala unaofuata sharia za Kiislamu. Limekuwa pia zikizilenga nchi jirani za Chad, Niger na Cameroon.

Idadi ya watoto wanaotumiwa na Boko Haram yaongezeka

Nigeria Boko Haram - Kinder als Selbstmordattentäter (picture-alliancce/AP Photo/J. Ola)

Moja ya mashambulizi yanayotajwa kufanywa na washambuliaji watoto wa Boko Haram kaskazini mwa Nigeria mwishoni mwa mwaka 2016.

Wakati huo huo, Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linasema kuwa Boko Haram imeongeza matumizi yake ya watoto kwenye mashambulizi ya kujitoa muhanga katika siku za hivi karibuni, ambapo mashambulizi ya tangu Januari mwaka huu yameshakaribia idadi sawa na yale yaliyofanyika kipindi chote cha mwaka jana.

UNICEF inasema mashambulizi 117 yalifanywa na watoto kwenye eneo la Ziwa Chad tangu mwaka 2014, ambapo asilimia 80 kati yao yalifanywa na wasichana, ambao baadhi ya wakati walikuwa wamepewa madawa ya kulevya kabla ya kujiripuwa.

"Vile tu kuonekana watoto karibu na masoko na vituo vya uangalizi kunazusha khofu," anasema Marie-Pierre Poirier, mkurugenzi wa UNICEF kwa mataifa ya Magharibi na Kati ya Afrika. Matokeo yake ni kuwa takribani watoto 1,500 walikamatwa na kuweka kizuizini mwaka jana katika mataifa ya Nigeria, Cameroon, Niger na Chad.

"Watoto hawa wenyewe ni wahanga, na sio watendaji wa uhalifu," alisema Poirier. "Kuwalazimisha ama kuwalaghai waingie kwenye matendo ya kihalifu kama haya ni jambo lisilosameheka." 

Watoto wametumika kufanya mashambulizi 27 ndani ya miezi mitatu ya mwaka huu, baada ya kuwa wamefanya mashambulizi kama hayo mara 30 mwaka jana. 

Ripoti hiyo ya UNICEF imetoka ikiwa ni mwaka wa tatu tangu Boko Haram kuwateka nyara wasichana 276 kwenye skuli ya Chibok, jimbo la Borno, wengi wao wakiwa hadi sasa hawajapatikana na kampeni ya kuwasaka ikiendelea.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AP
Mhariri: Josephat Charo