Barua kutoka Dar: Kuukaribisha 2021 na matarajio ya amani | Matukio ya Afrika | DW | 04.01.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Barua kutoka Dar: Kuukaribisha 2021 na matarajio ya amani

Tumeibuka tu kutoka mwaka utakaokumbukwa sana kwa janga lililotikisa ulimwengu wote, mabadiliko ya kisiasa na maandamano makubwa ya kudai haki katika jamii.

 

Dar es Salaam- Hali ya uchumi kwa watu barani Afrika imekuwa ngumu mnamo 2020. Mwaka umeisha huku maelfu ya familia katika miji na vijiji zikiwa zimepoteza hamu ya sherehe na wengi hawakuhisi kusherehekea kipindi hiki kama ilivyokuwa kawaida miaka mingine.

 Watanzania, hata hivyo, bado tuna sababu ya kuwa wachangamfu wakati nchi inapoanza mwaka mpya kwa matumaini ya maendeleo pande zote, haswa kutokana na kushuka kwa mfumuko wa bei.

Kulingana na Benki Kuu, mfumuko wa bei unatarajiwa kubaki katika kiwango cha asilimia 3.0 hadi asilimia 5.0 kwa kipindi chote cha 2020/2021. Mfumuko wa bei wa kila mwaka wa chakula na vinywaji visivyo vya kileo uliendelea kupungua 2020, ikionesha hali nzuri ya usambazaji wa chakula nchini.

Katika maeneo yenye ukorofi mbaya sana barani Afrika, hata hivyo, umwagaji damu unaendelea. Usafirishaji wa binadamu na mitandao ya biashara haramu inaendelea ambapo serikali zinashindwa kukataza uhalifu huo. Nchi zingine zimekuwa maarufu kwa usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya.

Juu ya hayo tunapaswa kuhoji kila kitu tunachokiona au kusikia juu ya ulimwengu unaotuzunguka kwa sababu ya kuenea kwa habari za upotoshaji wa makusudi.

Basi ni vipi tutahakikisha kuwa na haki katika mazingira haya ambapo tunapaswa kudumisha hatua za kutokaribiana kwa kuogopa maambukizi mabaya. Kinachosikitisha, jamii zetu nyingi hazizingatii uwazi na kukenea ufisadi.

Tansania Dar Es Salaam | Kariakoo Markt | Händler

Wananchi katika shughuli za biashara

Kwa kweli, ufisadi, katika aina zake zote zilizofichika, umekuwa maarufu katika jamii nyingi kuanzia mitaani, ngazi za kitaifa na kimataifa ambapo unazuia amani kuimarika. Ni shida ambayo inapaswa kushughulikiwa kutoka pande zote ili kuhakikisha amani ya ulimwengu na maisha bora.

Hapana budi kazi ianze kwa kusafisha tawala za umma, vikosi vya utekelezaji na kutunga sheria pamoja na mifumo ya haki katika kila nchi. Wanawake kwa vijana na wazee pia wanapiga kelele dhidi ya kukoseshwa fursa za kiuchumi kwa sababu ya ufisadi.

Wenye tamaa bado hutumia kila ujanja ili kuathiri maamuzi ya walio na mamlaka kwa kuwapa upendeleo.

Hali ngumu, hata hivyo, huongeza ufahamu wa umuhimu wa ushirikiano. Hakuna maoni yanayopingana juu ya mataifa makubwa na madogo kuunda kwa pamoja njia ya kufikia kile sote tunaamini kuwa ni mustakabali wetu.

Ulimwengu umekuwa ukifuatilia kwa makini matukio katika ardhi ya Mjomba Sam (Uncle Sam) wakati utawala mpya unajiandaa kuingia Ikulu mnamo Januari 2021.

 Lengo la mataifa makubwa sio tu juu ya mabadiliko ya walinzi na uteuzi unaofanywa na Rais mteule, bali ni juu ya ushirikiano wao na Marekani, wakizingatia masilahi yao na siasa za kijiografia.

Tansania Amtseid des Präsidenten John Pombe Magufuli

Rais John Magufuli akila kiapo cha muhula wa pili

Ni hapa uhusiano wa Ulaya na upande wa pili wa Bahari ya Atlantiki unalindwa ili kuhakikisha utulivu na ustawi. Uhusiano thabiti na wenye faida na Marekani una umuhimu sawa kwa Afrika na kwa ulimwengu wote. Barani Afrika, tunafahamu vizuri uhusiano duni wa utawala unaomaliza muda wake Marekani, kwa sababu ya dharau na kutoelewa bara hili na watu wake. Sera ya kigeni ya Rais Donald Trump haitaacha alama ya kudumu katika bara hili baada ya kuachia madaraka.

Ushirikiano wa Marekani na Ulaya umejikita katika maadili ya pamoja na masilahi ya kawaida. Inapaswa kuwa sawa pia kwa Afrika kama mizizi yake katika utamaduni na historia haikupotoshwa na viongozi na wale wanaodai kuwa waandishi wa fasihi juu ya Wamarekani wapya waliovuka Atlantiki, ikiwa pamoja na Waafrika.

Sasa ni wakati wa Umoja wa Afrika kuthibitisha umuhimu wa kimkakati wa ushirikiano wa bara hili na Amerika ya Kaskazini, Karibiani, Amerika Kusini na pia eneo la Pasifiki Kusini. Si ajabu watu wengi  hawafahamu kwamba Wafiji, ambao asili yao haikutokana na Wahindi, kwa mfano, wana asili yao Afrika.

Wanasema wenyewe asili ya mababu zao inaweza kupatikana karibu na Ziwa Tanganyika. Nilishangaa waliponiambia hadithi hii wakati tukila chakula cha nyumbani -- ndizi na viazi vikuu katika mji wa Nadi. Nilifurahia mlo huo ambao ni miongoni mwa mazao yaliyochukuliwa na mababu wa Wafiji wakati wakihama kutoka Afrika.  Nimekula chakula kilekile katika Amerika ya Kati na visiwa vya Karibiani ambako Waafrika walihamia pia.

Msimamo wa Afrika katika diplomasia ya pande nyingi na ushirikiano wa kimataifa katika muongo unaoanza sasa utakuwa na maana kubwa ikiwa utajumuisha uwezo wa Waafrika kupata suluhisho zao kwa changamoto za ulimwengu.

Lakini, tumejiandaa vipi kama zitatokea changamoto na athari kubwa katika uchumi zaidi ya zile tulizokumbana nazo mpaka sasa? Zinahitajika hatua za haraka kufanya uvumbuzi wa Kiafrika uonekane katika utendaji kazi, mazingira yetu yaruhusu uvumbuzi endelevu, uwazi udumishwe na sekta binafsi ipate fedha za hakika kwa ajili ya maendeleo.

Na Anaclet Rwegayura