Baraza la Usalama laidhinisha mkataba wa kusitisha vita Libya | Matukio ya Afrika | DW | 28.10.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Baraza la Usalama laidhinisha mkataba wa kusitisha vita Libya

Baraza la Usalama limeidhinisha mkataba wa kusimamisha mapigano nchini Libya.Limezitolea mwito pande hasimu kutekeleza kikamilifu mkataba huo.

Duru za kidiplomasia zinaelezea kuwa azimio kuhusu Libya linatarajiwa kupitishwa na Baraza la Usalama mnamo siku za usoni.Taarifa ya pamoja ya Baraza hilo imepongeza mkataba wa kusitisha mapigano nchini Libya uliotiwa saini mjini Geneva,Uswisi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka pande zote husika kuuheshimu na kuutekeleza kikamilifu.

Umoja wa mataifa umezihimiza pande hizo kuonyesha nia katika kutafuta suluhisho la kisiasa la mzozo kwenye vikao vitakavyoanza nchini Tunisia ifikapo Desemba 9.

Taarifa hiyo ya Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa limekumbusha pia umuhimu wa kuheshimu marufuku ya silaha ya mwaka 2011 na limeziomba nchi za nje na pande zinazohusika nchini Libya kujiepusha kujiingiza kati kwenye masuala ya ndani ya taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

Oktoba 23, pande hasimu nchini Libya zilitia saini mkataba wa kudumu wa kusitisha mapigano,mjini Geneva,baada siku tano za mazungumzo chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa. Hatua ambayo imepongezwa na Umoja wa Mataifa katika juhudi za kukomesha umwagikaji wa damu katika nchi hiyo iliyokumbwa na machafuko kwa takriban miaka kumi sasa.

Kuondoka kwa mamluki kutoka nje ?

Stephanie Williams, mjumbe mwandamanizi wa Umoja wa Mataifa anayeshugulikia Libya

Stephanie Williams, mjumbe mwandamanizi wa Umoja wa Mataifa anayeshugulikia Libya

Stephanie Williams, mjumbe mwandamanizi wa Umoja wa Mataifa anayeshugulikia Libya, aliyaita makubaliano hayo kuwa ya kihistoria baada ya mapigano ya miaka kadhaa yaliyoigawanya Libya katika pande mbili. Williams amesema makundi yenye silaha na vikosi vya kijeshi vimekubali kurejea kwenye kambi zao na kwamba makubaliano yaliyofikiwa yataanza kutekelezwa mara moja.

Pamoja na hatua nyingine, makubaliano hayo yanazingatia kuondolewa kwa mamluki wa kutoka nje na kuwezesha kufanyika mazungumzo mwezi ujao ili kutafuta suluhisho la kudumu. Libya ilitumbukia katika vurumai baada ya nchi za NATO kuivamia nchi hiyo mnamo mwaka 2011 na kumwondoa kiongozi wake kanali Muammar Gaddaffi aliyetawala kwa muda mrefu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema makubaliano yaliyofikiwa ni muhimu sana, hata hivyo ameeleza kuwa juhudi zaidi zinahitajika.