Barack Obama awasili Ufaransa | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 25.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Barack Obama awasili Ufaransa

Mgombea kiti cha urais kutoka chama cha demokrate nchini Marekani Barack Obama amewasili mjini Paris Ufaransa kwa mazungumzo na rais Nicolas Sarkozy kabla ya kuendelea na ziara yake mjini London Uingereza.

Seneta Barack Obama

Seneta Barack Obama

Barack Obama amewasili kwenye uwanja wa ndege wa Paris-Le Bourget. Mara tu baada ya kuwasili, Barack Obama amesafirishwa moja kwa moja katika ikulu ya rais wa Ufaransa, Champs Elysées kwa mazungumzo na rais Nicolas Sarkozy ambae ndio alikuwa amerudi mjini Paris akitokea mjini Bordeaux magharibi mwa Ufaransa kushiriki katika mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika juu ya mzozo wa Zimbabwe. Miongoni mwa maswala yatakayozungumziwa kati ya rais Nicolas Sarkozy na Barack Obama ni pamoja na uhusiano kati ya pande mbili za bahari ya Atlantiki yaani Amerika na Ulaya na uhusiano kati ya Marekani na Ufaransa.

Ziara ya Barack Obama nchini Ufaransa itakuwa ya masaa machache na itakamilishwa na mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na rais Nicolas Sarkozy. Rais Nicolas Sarkozy alimtaja Barack Obama kuwa ni ´´rafiki yake´´ katika mahojiano na gazeti la hapo Ufaransa la Le Figaro. Wanasiasa hao wawili wameshakutana kwa mazungumzo mjini Washington Marekani mwaka 2006 kabla ya Nicolas Sarkozy kuteuliwa kuwa rais wa Ufaransa.

Barack Obama amefika Ufaransa akitokea Ujerumani ambapo hapo jana alitoa hotuba iliyojaa hamasa na ambayo ilikaribishwa vizuri na raia na serikali ya Ujerumani. Serikali ya Ujerumani imesema hotuba aliyeyitoa Barack Obama mbele ya ummati mkubwa wa watu zaidi ya laki mbili mjini Berlin ilitoa ishara nzuri kwa Ulaya kama anavyoelezea hapa msemaji wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Ulrich Wilhelm: ´´Kwa mtazamo wa Kansela wa Ujerumani na serikali yake, hotuba ya Obama ni ishara nzuri kwa bara la Ulaya. Obama alisisitiza kwamba tutaweza kukabiliana na changamoto za karne hii ya 21 ikiwa tutapitia katika ushirikiano wa kimataifa´´.

Barack Obama alitoa hotuba yake mjini Berlin baada ya kukutana kwa mazungumzo na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri wa mambo ya kigeni Frank-Walter Steinmeier katika hatua ya kwanza ya siku tatu barani Ulaya.

Ziara ya Barack Obama ya zaidi ya wiki moja Mashariki ya kati na hapa Ulaya imefana. Barack Obama anampita mara tisa hivi mshindani wake kutoka chama cha republikan John Mc Cain kuhusu kiwango cha michango ya kifedha ya raia wa Marekani waishio Ulaya kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi. Raia wa Marekani waishio nchini Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wameshatoa milioni 1 za dola za kimarekani ikiwa ni sawa na 640,000 za Euro kwa ajili ya Barack Obama wakati John Mc Cain ameshapata tu laki 1 na nusu za dola ikiwa ni sawa na alfu 95 za Euro tu.
 • Tarehe 25.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ejnl
 • Tarehe 25.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ejnl
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com