Barack Obama atarajiwa kuwasili Ufaransa | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 25.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Barack Obama atarajiwa kuwasili Ufaransa

Mgombea kiti cha urais kutoka chama cha demokrate nchini Marekani Barack Obama, anatarajiwa kuwasili katika mji mkuu wa Ufaransa Paris kwa mazungumzo na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy kabla ya kuendelea Uingereza.

Seneta Barack Obama jana mjini Berlin Ujerumani

Seneta Barack Obama jana mjini Berlin Ujerumani

Barack Obama na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, wanatarajia kuzungumzia juu ya maswala muhimu yanayoikabili dunia ikiwa ni pamoja na changamoto za usalama, matatizo ya ushirikiano kati ya bara la Amerika na Ulaya na matatizo ya uchumi wa dunia.

Rais wa Ufaransa alipania katika mhula wake kuboresha uhusiano kati ya Marekani na nchi yake na ushirikiano kati ya nchi za bara la Amerika na Ulaya kwa jumla. Barack Obama anaitembelea Ufaransa wakati utafiti wa maoni ya raia umeonyesha kuwa raia wengi wa Ufaransa wangependelea Barack Obama awe rais wa Marekani siku zijazo.

Jana akiwa mjini Berlin mji mkuu wa Ujerumani, Barack Obama alisema mbele ya watu zaidi ya laki mbili kwamba ikiwa atachaguliwa atajitahidi kuimarisha uhusiano kati ya nchi za bara la Amerika na nchi za Ulaya na ustawi wa jamii duniani kwa kuondoa kuta zinazogawa sasa jamii hizo:´´Kuta kati ya washirika wa zamani katika pande zote za Bahari ya Atlantiki haziwezi kubaki, kuta kati ya nchi tajiri na nchi masikini haziwezi kubaki, kuta kati ya makabila na koo, wenyeji na wahamiaji, wakristu, waislamu na wayahudi haziwezi kubaki. Hizi ndizo kuta tunapaswa kuvunja´´.

Hotuba yake hiyo mjini Berlin ilikuwa na hamasa kubwa miongoni mwa raia wa Ujerumani ambao asili mia 72 wanamuunga mkono Barack Obama. Kwa jumla raia nchini Ulaya wanaunga mkono Barack Obama katika sera zake za nchi za nje ikiwa ni pamoja na kuifunga kambi ya Guantanamo nchini Cuba ambayo sasa imegeuka jela ya mateso dhidi ya watuhumiwa wa ugaidi, kupambana na ongezeko la silaha za kinyuklia, mabadiliko ya hali ya hewa na kuimarisha mpango wa kibiashara.

Ziara hiyo ya Barack Obama katika nchi za Mashariki ya kati na Ulaya ilimpa fursa ya kuyajadili maswala yanayoikabili dunia wakati huu na kuwashawishi wapiga kura nchini Marekani juu ya kipaji chake kuiongoza nchi. Barack Obama alisema Marekani haina uwezo wa kuyasuluhisha peke yake matatizo yanayoikabili kwa wakati huu. Ziara hiyo ya Barack Obama nchini Ufaransa itadumu masaa machache. Baada ya kukutana kwa mazungumzo na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy , Barack Obama anatarajiwa kuwa na mkutano na waandishi wa habari kabla ya kuendelea na ziara yake nchini Uingereza kukamilisha ziara yake ya zaidi ya wiki moja katika nchi za kigeni.
 • Tarehe 25.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EjYp
 • Tarehe 25.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EjYp
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com