1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yasikitishwa na vurugu dhidi ya wahamiaji wa kiafrika

Sylvia Mwehozi
27 Juni 2022

Mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameeleza kushtushwa kwake na vitendo vya vurugu na kudhalilisha dhidi ya wahamiaji wa kiafrika.

https://p.dw.com/p/4DIlN
Spanien Melilla | Migranten in der spanischen Nordafrika-Exklave Melilla
Picha: Javier Bernardo/AP/picture alliance

Mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameeleza kushtushwa kwake na vitendo vya vurugu na kudhalilisha, dhidi ya wahamiaji wa kiafrika. Kauli yake hiyo inahusu vurugu zilizojitokeza mwishoni mwa juma, baada ya wahamiaji 23 kupoteza maisha. Wahamaji hao walikuwa wanajaribu kuvuka mpaka kutoka Morocco kwenda Uhispania. Takriban wahamiaji 2,000 walivamia mpaka wenye vizuizi vingi kati ya eneo la Morocco la Nador na eneo la Uhispania la Melilla siku ya Ijumaa. Mahamat ametaka uchunguzi wa haraka ufanyike juu ya tukio hilo na kuzitaka nchi kukumbuka wajibu wao chini ya sheria za kimataifa. Sheria hizo zinataka mataifa yote kuwatendea haki wahamiaji wote kwa utu na kutanguliza usalama wao na haki za binadamu, huku zikijiepusha na matumizi ya nguvu kupita kiasi.