1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad ashiriki mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Mohammed Khelef
19 Mei 2023

Rais Bashar al-Assad wa Syria yuko nchini Saudi Arabia kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu baada ya zaidi ya muongo mmoja wa kutengwa na jumuiya hiyo kutokana na vita nchini mwake.

https://p.dw.com/p/4RZQv
Vor dem 32. Arabischen Gipfeltreffen in Saudi Arabien Baschar al-Assad, Präsident von Syrien
Picha: SPA/AFP

Kwa mujibu wa shirika la habari la Syria (SANA), Rais Assad aliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Abdulaziz mjini Jeddah jioni ya Alkhamis (Mei 18) kushiriki mkutano huo ulioanza Ijumaa (Mei 19).

Kituo cha televisheni cha Saudi Arabia, Al-Akhbariya, kilionesha picha za Assad akishuka ndege huku akitabasamu na akilakiwa na naibu gavana wa mkoa wa Makka ambako ndiko uliko mji wa Jeddah, Mwana Mfalme Badr bin Sultan. 

Soma: Rais wa Syria kuhudhuria mkutano wa kilele Saudi Arabia

Gazeti la al-Watan linalomilikiwa na serikali ya Syria liliandika kuwa Assad alianza kukutana na viongozi kadhaa wa mataifa ya Kiarabu kwenye mazungumzo ya pande mbili kuanzia jioni ya Alkhamis na aliendelea kufanya hivyo asubuhi ya Ijumaa. 

Mara ya mwisho kwa Syria kushiriki mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilikuwa ni mwaka 2010 nchini Libya.

Mabadiliko kwenye ulimwengu wa Kiarabu

Vor dem 32. Arabischen Gipfeltreffen in Saudi Arabien Baschar al-Assad, Präsident von Syrien
Rais Bashar al-Assad wa Syria (katikati) akikaribishwa mjini Jeddah.Picha: SANA/REUTERS

Ushiriki huu wa Assad kwenye mkutano wa kilele wa Jumuiya hiyo ya Nchi za Kiarabu unaashiria hatua kubwa zilizopigwa kwenye kurejesha mahusiano kati ya Syria na majirani zake, zinazoongozwa na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu licha ya upinzani kutoka kwa viongozi wengine wa Kiarabu.

Soma: Syria yaomba mataifa ya Kiarabu kuwekeza nchini humo.

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilisitisha uanachama wa Syria mwezi Novemba 2011 kufuatia ukandamizaji mkali dhidi maandamano ya umma uliopelekea vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo hadi sasa vimeshauwa watu laki tano na kuwasababishia mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi wa ndani na nje.

Saudi Arabia na mataifa mengine ya Kiarabu ama yalivunja kabisa ama kupunguza kiwango cha mafungamano yake na utawala wa Assad, huku Saudi Arabia ikijitokeza wazi wazi kutaka aondolewe madarakani.

Kukaribishwa tena kwa Assad

Vor dem 32. Arabischen Gipfeltreffen in Saudi Arabien Baschar al-Assad, Präsident von Syrien
Rais Assad wa Syria baada ya kuwasili nchini Saudi Arabia.Picha: Mosa Al Kathami/Saudi Press Agency/dpa/picture alliance

Lakini mapema mwezi huu, Jumuiya hiyo yenye mataifa wanachama 22 iliikaribisha tena Syria na Saudi Arabia ilimualika rasmi Assad kwenda mjini Jeddah, ikiwa sehemu ya mkururo wa hatua za kidiplomasia ambazo zimekuwa zikilitikisa eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati kwa miezi ya hivi karibuni. 

Serikali za mataifa ya eneo hilo zimekuwa zikimkaribisha tena Assad tangu ilipobainika wazi kwamba ameweza kushinda kwenye vita dhidi ya makundi ya waasi na ya kigaidi kwa msaada mkubwa wa Urusi na Iran.

Soma zaidi: Rais wa Syria aalikwa katika mikutano mikuu miwili

Mnamo mwaka 2018, Umoja wa Falme za Kiarabu ilirejesha mahusiano yake na Syria, na tangu hapo umejibebesha jukumu la kuiombea Damascus kukubalika tena kwa majirani zake wa Kiarabu. 

Assadaaliitembelea nchi hiyo mwaka jana na tayari amealikwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika Dubai baadaye mwaka huu.

Vyanzo: Reuters, AFP