Argentina yalenga kumaliza kiu ya miaka 28 | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 22.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Argentina yalenga kumaliza kiu ya miaka 28

Kuimarika kwa mchezo wa Lionel Messi na uelekezi wa mkufunzi Alejandro Sabella vimewaacha wengi kuamini kuwa Argentina wako tayari kumaliza kiangazi cha muda mrefu cha kushinda Kombe la Dunia kwa mara ya tatu

Miamba hao wa Amerika ya kusini kila mara wamepigiwa upatu kufanya vyema katika vinyang’anyiro vya karibuni vya Kombe la Dunia, lakini wao hunyauka chini ya shinikizo punde tu tamasha lenyewe linapoanza.

Vikosi vya mfululizo vilivyojaa wachezaji wa kimataifa wenye vipaji vinashindwa kupata matokeo bora, kumaanisha kuwa miaka 28 imepita tangu timu ya Argentina iliyoongozwa na Diego Maradona iliponyanyua Kombe la Dunia, nchini Mexico mwaka wa 1986. Lakini kuna dalili kuwa mwaka huu mambo yanaweza kuwa tofauti. Safari ya Argentina kufuzu katika tamasha la mwaka huu imekuwa ya kuridhisha ikilinganishwa na ile ya mwaka wa 2010 nchini Afrika Kusini. Walijikatia tikiti ya Brazil wakiwa na mechi mbili zilizosalia kuchezwa, wka kuwararua Paraguay magoli matano kwa mawili kwa kuonyesha mchezo wa kushambulia ambao unatuma onyo kwa wapinzani wao wa Kundi F, Iran, mabingwa wa Afrika Nigeria na Bosnia- Harcegovina.

Messi aliisaidia Brazil kujikatia tikiti kwa urahisi

Kocha wa timu ya taifa ya Brazil - SELECAO Alejandro Sabella ameyaweka matumaini yake kwa Lionel Messi

Kocha wa timu ya taifa ya Brazil - SELECAO Alejandro Sabella ameyaweka matumaini yake kwa Lionel Messi

Jambo muhimu katika safari ya Argentina lilikuwa hali nzuri ya nyota wa Barcelona Lionel Messi, aliyefanya vyema katika jukumu la unahodha alilopewa na Sabella ambaye alipewa majukumu ya ukocha mwaka wa 2011.

Messi alikuwa mfungaji bora wa Argentina katika awamu ya kufuzu, kwa kutikisa nyavu mara 10. Hali ya mchezo wa nyota huyo katika klabu yake haijakuwa nzuri katika siku za karibuni, na umeathiriwa na majeraha katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, lakini mchezo wake katika jukwaa la kimataifa ni ushahidi kwa imani ambayo Sabella amemwekea nahodha wake huyo. Tofauti na Maradona – ambaye alishindwa kuiwekea uwiano safu ya mashambulizi katika dimba lililopita la Kombe la Dunia kwa kumjumuisha mshambuliaji Carlos Tevez, Sabella amejenga kikosi chake kwa kutumia nguzo ya Messi.

Sabella anasema lazima wamfanye Messi ajihisi kuwa sawa na kufikiria kilicho bora kwa timu. Matokeo yake, Tevez hajaichezea timu ya taifa tangu dimba la Copa America mwaka wa 2011, wakati Argentina ilipobanduliwa nje na Uruguay katika robo fainali. Hata hivyo, La Albiceleste siyo tu timu ya mtu mmoja. Kikosi hicho cha Sabella kina nyota kadhaa ambao wanaweza kujumuishwa kwa urahisi katika vikosi vingine vya kwanza katika Kombe la Dunia, kama vile mshambuliaji wa Napoli Gonzalo Higuain, wachezaji wa Manchester City Sergio Aguero na Pablo Zabaleta, beki na kiungo wa Barca Javier Mascherano na mshambuliaji wa Real Madrid Angel Di Maria.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com