1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMali

Aliyelituhumu jeshi kwa unyanyasaji nchini Mali akamatwa

4 Machi 2024

Afisa mmoja wa jeshi la Mali ambaye kitabu chake kilichochapishwa hivi karibuni kimewatuhumu wanajeshi kuwatesa raia, amekamatwa kwenye mji mkuu Bamako.

https://p.dw.com/p/4d7r9
Mali | Bamako
Mali imekuwa ikikabiliwa na uasi wa makundi ya itikadi kali hali iliyochochea mapinduzi ya kijeshi mnamo Agosti, 2020 Picha: AP Photo/picture alliance

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la AFP likinukuu chanzo kimoja cha kijeshi kinachofahamu kile kilichotokea. Pia mwanafamilia mmoja amethibitisha taarifa hizo.

Inaarifiwa, Kanali Alpha Yaya Sangare, alitiwa nguvu siku ya Jumamosi, siku moja baada ya Wizara ya Ulinzi ya Mali kutoa tamko la kukosoa sehemu ya kurasa za kitabu cha afisa huyo ikisema "zimetoa tuhuma za uongo" dhidi ya jeshi.

Katika kitabu chake alichokipa jina la "Mali na changamoto ya ugaidi barani Afrika", kanali Sangare alinukuu ripoti za mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu juu ya unyanyasaji unaofanywa na jeshi dhidi ya raia katika operesheni zake za kupambana na ugaidi.

Madai hayo inaonesha hayakuufurahisha utawala wa kijeshi unaoitawala nchi hiyo ya Afrika Magharibi tangu mwaka 2020.