1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabaab waanza mashambulizi ya kuvizia Kismayu

Admin.WagnerD3 Oktoba 2012

Vikosi vya Umoja wa Afrika na vifaru viliingia mji wa Kismayu Jumanne, lakini wanamgambo wa Al-Shabaab walionya kuwa wataurejesha mji huo mikononi mwao, na kusema kwamba walihusika na mripuko wa bomu katika mji huo.

https://p.dw.com/p/16JEl
Mwanajeshi wa Ethiopia akipiga Redio Kol makao makuu baada ya kuingia mji wa Kismayu tarehe 1, Oktoba.
Mwanajeshi wa Ethiopia akipiga Redio Kol makao makuu baada ya kuingia mji wa Kismayu tarehe 1, Oktoba.Picha: picture-alliance/dpa

Mripuko huo wa Jumanne unaonyesha jinsi gani kundi hilo lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-qaeda lina uwezo wa kurudisha mashambulizi ya kuvizia na linaendelea na mashambulizi ya mara kwa mara katika maeneo mengine ya mjini ambako limeondoka kutokana na shinikizo la kijeshi, ikwemo katika mji mkuu Mogadishu. Msemaji wa shughuli za kijeshi za Al-Shabaab, Sheikh Abdiasis Abu Musab, alisema bomu lililoripuka lilitegwa katika jengo la ofisi ya utawala ya wilaya ambako kuna vikosi vya Somalia, na kuonya kuwa mashambulizi mengine yatafuata.

Vikosi vya washirika vikiwa katika kituo mjini Shalambood, karibu na Marka, walioiteka mwezi Agosti.
Vikosi vya washirika vikiwa katika kituo mjini Shalambood, karibu na Marka, walioiteka mwezi Agosti.Picha: picture-alliance/dpa

"Huu ni utambulisho tu wa mashambulizi yanayokuja huko mbele," aliliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters, na kuongeza kuwa wanamgambo wake wamefanikiwa kuwauwa watu wengi katika shambulio hilo. Lakini serikali ilisema hakukuwa na madhara katika shambulio hilo. Majeshi ya Kenya, yanayopigana chini ya mwavuli wa Umoja wa Afrika, yaliingia mjini Kisamyu kwa mara ya kwanza siku ya Jumanne, baada ya kuanzisha operesheni iliyowalazimu Al-Shabaab kuukimbia mji huyo ijumaa wiki iliyopita. Vikosi hivyo vya Kenya viliwafuata mamia ya wanajeshi wa serikali na vikosi vya wanamgambo washirika waliyoingia mjini humo siku ya jumatatu.

Uwezo wa Al-Shabaab haujulikani

Ni vigumu kupima nguvu ya Al-Shabaab. Msemaji wa vikosi vya serikali ya Somalia, Mahmoud Farah, alisema kati ya wapiganaji alfu 4 na alfu 5 walikuwa wamejificha katika mikoa ya kusini ya Juba. Mamia ya wapiganaji wa kigeni pia walijiunga na kundi hilo wakati lilipokuwa katika kiwango cha juu cha ushawishi,wakitokea Afghanistan, Pakistan, Kenya, Tanzania na hata Marekani na Uingereza, kwa mujibu wa serikali iliyomaliza muda wake. Lakini mshauri moja wa masuala ya usalama aliyeko mjini Nairobi alisema wapiganaji wengi wa kigeni waliondoka baada ya kuona kuwa nafasi yao ilikuwa inapungua, hasa baada ya mafanikio ya vikosi vya Umoja wa Afrika katika miezi 14 iliyopita.

Wanajeshi wa Uganda waliyoko katika vikosi vya AMISON wakiwa kazini nchini Somalia.
Wanajeshi wa Uganda waliyoko katika vikosi vya AMISON wakiwa kazini nchini Somalia.Picha: picture-alliance/dpa

Baada ya kusalimu kwa mji wa Kismayu, inatarajiwa pia idadi ya waasi watakaojisalimisha itaongezeka na wachambuzi wanasema watakaosalia ni wale wenye msimamo mkali tu. Uwezo wa Al-Shabaab kuendesha kampeni ya muda mrefu ya mashambulizi ya kuvizia utategemea kwa kiasi kikubwa ufanisi wa utawala mjini Mogadishu kuweka mfumo wa tawala za mikoa unaokidhi malsahi kinzani ya koo kusini mwa Somalia. Mshauri huyo wa masuala ya usalama alisema kama kutakuwa na koo ambazo zintaweza, basi Al-Shabaab watapata washirika katika koo hizo, lakini kama koo zote zitashirikishwa kisawa sawa, itakuwa vigumu kwa kundi hilo kijipenyeza tena ndani ya Kismayu.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Othman Miraj