Afrika Kusini yahamisha mechi kwa heshima ya Senzo | Michezo | DW | 31.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Afrika Kusini yahamisha mechi kwa heshima ya Senzo

Afrika Kusini imeruhusiwa kuuhamisha mpambano ujao wa kufuzu katika dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika na kuuandaa katika mji alikozaliwa nahodha wa timu ya taifa Senzo Meyiwa aliyeuawa mwishoni mwa wiki.

Rais wa Shirikisho la Kandanda Afrika Kusini - SAFA Danny Jordaan Jordaan amesema wamepwa kibali maalum na Shirikisho la Kandanda Afrika - CAF kubadilisha uwanja wa mchuano wa mwezi ujao dhidi ya Sudan.

Jordaan aliyasema hayo katika ibada ya mazishi ya mlinda lango huyo pamoja na wanamichezo wengine wawili wa Afrika Kusini ambao walipoteza maisha yao katika siku chache zilizopita. "Tumewapoteza mashujaa watatu wa michezo Afrika Kusini, ndondi, riadha na kandanda. Hivyo tumekuja hapa kutoa heshima, kusherehekea mafanikio yao na kuwakumbuka. Senzo alikuwa mchezaji wa kipekee na mchango wake na uongozi wake katika timu kila mara ulionekana kwa wachezaji wote, na ndio maana kifo chake kimetuvunja moyo".

Mwanariadha bingwa wa zamani wa Afrika Kusini Mbulaeni Mulaudzi aliuawa katika ajali ya gari siku ya Ijumaa wakati bondia mwanamke Phindile Mwelase alifariki dunia siku ya Jumamosi. Pia Jordaan alisema sanamu la Meyiwa litajengwa mbele ya makao makuu ya Shirikisho la kandanda la Afrika Kusini.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Josephat Charo