Afrika Kusini: wasiwasi juu ya ongezeko la virusi vya corona | Matukio ya Afrika | DW | 23.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Afrika Kusini: wasiwasi juu ya ongezeko la virusi vya corona

Idadi jumla ya vifo vya kawaida Afrika Kusini imeongezeka kwa asilimia 60 katika wiki za hivi karibuni, na kuashiria idadi kubwa zaidi ya vifo vinavyotokana na virusi vya corona kuliko ile iliyoripotiwa rasmi.

Afrika Kusini imerekodi ongezeko la karibu asilimia 60 ya idadi jumla ya vifo vya kawaida katika wiki za hivi karibuni na kuashiria idadi kubwa zaidi ya vifo vinavyotokana na virusi vya corona kuliko ile iliyoripotiwa rasmi.

Ripoti ya baraza la utafiti wa matibabu la Afrika Kusini (SAMRC) iliyotolewa Jumatano jioni, imesema kuwa katika wiki chache zilizopita, idadi hiyo imeonesha ongezeko la kasi na kwamba kufikia wiki ya pili ya mwezi Julai, kulikuwa na asilimia 59 ya vifo zaidi kutokana na sababu za kawaida mbali na idadi ambayo ingetarajiwa kutokana na historia ya takwimu.

Ripoti  ya baraza hilo linalofadhiliwa na serikali lakini kufanya shughuli zake kwa njia huru, imetolewa huku wizara ya afya nchini humo ikitangaza ongezeko la vifo 572 linalotokana na virusi vya corona  katika muda wa saa 24.

Afrika Kusini ndilo taifa lililoathirika vibaya zaidi kutokana na virusi vya corona barani Afrika  na miongoni mwa mataifa matano duniani yanayoongoza kwa visa vya maambukizi vilivyothibitishwa kwa kuwa na maambukizi 394,948 yalioripotiwa kufikia sasa na vifo 5,940.

Kiwango cha vifo bado kiko chini, karibu asilimia 1.5, kulingana na taarifa za kila siku zilotolewa Jumatano na wizara ya afya.

Jukumu la SAMRC ni kufanya utafiti juu ya mwenendo wa magonjwa na kubaini sababu kuu za vifo nchini.

Chanzo: AFPE