Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 13.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya Rais wa Nigeria kuwania muhula wa pili. Kufikishwa mahakamani kwa rais Zuma na juu ya jeshi la Ujerumani kutoa mafunzo ya kijeshi nchini Mali na nchi zingine za eneo la Sahel.

Süddeutsche Zeitung

Makala ya gazeti la Süddeutsche juu ya uamuzi wa rais wa Nigeria Mohammed Buhari wa kutaka kuwania muhula wa pili wa urais, gazeti hilo linasema Buhari amejaribu kuchukua hatua ili kuufufua uchumi, kupambana na ufisadi na kuwakabili magaidi wa Boko Haram. Lakini hatua hizo hazikuwa ndefu. Na juu ya uamuzi wa rais huyo wa kuwania muhula wa pili, Süddeutsche Zeitung linaeleza.

Rais Buhari mwenyewe amesema amefikia uamuzi huo kutokana na maombi ya wananchi wake lakini kwa kweli nchini kote hakuna kilichoonyesha dalili ya maombi hayo. Kilichoonekana ni nasaha za kumshauri asiendelee madarakani. Na hata mkewe Aisha ana mtazamo huo huo. Wananchi wengi wa Nigeria wanajiuliza iwapo Buhari anazo nguvu za kutosha za kumwezesha kuyatimiza majukumu yake.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linatupeleka nchini Afrika Kusini ambako rais wa hapo awali Jacob Zuma alifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ufisadi. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba chama chake cha ANC kinakereka na kesi hiyo. Na linaeleza kuwa utawala wa Zuma uliandamwa na kashfa nyingi zilizoharibu jina la Afrika Kusini. Lakini Zuma anahisi kuwa anaonewa. Chimbuko la tuhuma za ufisadi zinazomkabili rais huyo wa Afrika Kusini ni pamoja na biashara ya silaha aliyofanya mnamo mwaka 1999 na kampuni moja ya Ufaransa  wakati alipokuwa makamu wa rais.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma (Reuters/N. Bothma)

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma

Hata hivyo tuhuma za ufisadi hazitaishia kwa Zuma tu. Gazeti hilo la die tageszeitung linasema alipokuwa madarakani Zuma alijenga urafiki wa karibu sana na ndugu watatu wa familia ya Gupta ambao pia wanakabiliwa na tuhuma za rushwa. Gazeti hilo linakumbusha kwamba Zuma aliandamwa na mashtaka mengi, lakini kila mara aliweza kunusurika na yote.

Frankfurter Allgemeine

Baraza la mawaziri la nchini Ujerumani limepitisha uamuzi wa kuendeleza mpango wa kutoa ushauri na mafunzo ya kijeshi nchini Mali na katika nchi nyingine kadhaa za eneo la Sahel. Serikali ya Ujerumani pia imeamua kuendeleza harakati za wanajeshi  wake za kupambana na maharamia kwenye pembe ya Afrika.

Wanajeshi wa Ujerumani (picture-alliance/dpa/M. Kappeler)

Wanajeshi wa Ujerumani

Juu ya uamuzi huo gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema, wanajeshi wa Ujerumani karibuni tu watautekeleza mpango wa kutoa mafunzo na ushauri kwa majeshi ya Mauritania, Niger na Chad ili kusaidia katika harakati za kupambana na ugaidi. Uamuzi wa kuongeza muda wa majukumu hayo katika nchi hizo za Afrika unatokana na azimio la baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Uwepo wa wanajeshi ya Ujerumani chini ya mpango wa Umoja wa Ulaya umechangia katika kuleta tija.

Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba mnamo mwaka 2011 meli za mizigo zilishambuliwa mara 176, na nyingine 25 zilitekwa nyara na maharamia kwenye bahari za Hindi na ile Shamu. Lakini katika miaka mitano iliyopita mikasa kama hiyo ilikuwa michache sana.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche limeandika makala nyingine juu ya teknolojia inayowanufaisha akina mama huko nchini Malawi. Gazeti hilo linatufahamisha kwamba wajasiriamali wawili wameanzisha kampuni inayoitwa Mamabird.

Mwanamke wa Kimalawi (DW)

Mwanamke wa Kimalawi

Kampuni hiyo inatengeneza teknolojia kwa ajili ya kuwasaidia wanawake katika sehemu za mashambani nchini Malawi. Wajasiramali hao wanatengeza ndege ndogo zinazoruka bila ya rubani kwa ajili ya kusafirishia dawa, mahitaji mengine ya tiba na chakula, hasa kwa ajili ya wanawake wajawazito.

Waanzilishi wa kampuni hiyo ya Mamabird  Eugene Maseya naThomas Lauzon wamesema lengo ni kuyaboresha maisha ya akina mama wa mashambani nchini Malawi ambako kati ya asilimia 60 na 80 ya watu wanaishi katika sehemu hizo.

Gazeti hilo la Süddeutsche limemnukulu mwanzilishi mwenza Eugene Maseya akieleza kuwa katika sehemu hizo za mashambani mtu anapaswa kutembea mwendo wa kilometa zaidi ya 10 kabla ya kuonana na daktari au kufika hospitali.

Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: