Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 26.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Miongoni mwa yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika mnamo wiki hii ni pamoja na mauaji ya kimbari ya Waherero na Wanama yaliyofanywa na wakoloni wa Kijerumani nchini Namibia.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche limeandika kwamba serikali ya Ujerumani inapinga kuilipa fidia Namibia lakini kwa kufanya hivyo hadhi yake imeharibika duniani na hasa baada ya watu wa makabila ya Herero na Nama kuwasilisha mashtaka dhidi ya Ujerumani tarehe 5 Januari mwaka uliopita. Ujerumani yenyewe iliweka kipimo cha juu kabisa katika kubainisha mauaji ya kimbari yaliyotokea katika historia duniani, kama vile ilivyoyatambua mauji ya halaiki ya  watu wa Armenia.

Rais wa zamani wa Ujerumani Joachim Gauck (picture-alliance/dpa)

Rais wa zamani wa Ujerumani Joachim Gauck

Gazeti hilo la Süddeutsche linakumbusha katika makala yake kwamba aliyekuwa rais wa Ujerumani Joachim Gauck ndiye aliyesema kwamba kuishughulikia historia ya uhalifu kama huo ndiyo msingi wa jamii ya kisasa na ya kidemokrasia. Gazeti hilo linasema  mpaka leo Ujerumani inakataa kuyatambua muaji ya Waherero yaliyofanywa na wakoloni wa Kijerumani katika karne iliyopita. Na linauliza kwa nini panahitajika mazungumzo ili kuyatambua mauaji hayo wakati ilipohusu yale ya Waarmenia bunge la Ujerumani liliyatambua bila ya mazungumzo na Uturuki? Lakini tofauti na Ujerumani.

Frankfurter Allgemeine

Ufaransa imeikubali dhima yake ya ukoloni barani Afrika. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaeleza katika kurasa zake kwamba katika hotuba aliyoitoa kwa wanafunzi wa chuo kikuu   cha Ouagadougou, nchini Burkina Faso rais wa Ufaransa  Emmanuel Macron aliishangaza dunia jinsi alivyokiri kwa  uwazi juu ya uhalifu uliotendwa na wakoloni wa Kifaransa  barani Afrika.  Katika hotuba yake Marcron alisema ni jambo lisiloeleweka kwa nini sanaa na turathi za Afrika zionyeshwe katika mji wa Paris na mingine ya baranai Ulaya ? Kwa nini zisionyeshwe katika miji ya Lagos, Dakar au Cotonou?

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (Reuters/E. Laurent)

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron

Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linafahamisha kwamba rais Macron anataka hatua zichukuliwe ili, mnamo kipindi cha miaka mitano ijayo sanaa na turathi za utamaduni wa Afrika zirudishwe kwa Waafrika wenyewe.

Hata hivyo  gazeti  la Frankfurter  Allgemeine  linasema, bila ya kuwekwa taratibu za kimataifa zoezi hilo halitaweza kutekelezwa. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba rais wa Ufaransa  Macron amechukua hatua ya kwanza muhimu, lakini hilo siyo suluhisho. Amekitonesha kidonda tu.

Süddeutsche Zeitung

Jee rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ni mtetezi wa mageuzi au ni mtetezi wa kungwi wake Robert Mugabe? Swali hilo linaulizwa katika makala nyingine ya gazeti la Süddeutsche mnamo wiki hii.

Zimbabwe sasa inaonekana kana kwamba ni nchi nyingine kabisa, tofauti ni jinsi ilivyokuwa hadi mnamo miezi ya hivi karibuni.Takriban kila siku vyombo vya habari vinaripoti juu ya tuhuma zaufisadi zinazowakabili maafisa wa serikali ya chama cha ZANU PF, aidha  kila siku rais mpya wa nchi hiyo Emmarson Mnangagwa anazungumzia juu ya mipango juu ya kuijenga Zimbabwe mpya. Vyombo vya habari pia vinaripoti juu ya mipango ya kuufufua uchumi na juu ya kuitishwa haraka,  uchaguzi huru na wa haki baada ya miaka 37 ya utawala  wa Robert Mugabe.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa (Reuters/P. Bulawayo)

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa

Hata hivyo gazeti hilo la Süddeutsche linasema viongozi waliopo madarakani nchini Zimbabwe ni wale wale wanaotoka kwenye zizi moja. Gazeti hilo linakumbusha kwamba rais Mnangagwa alimtumikia Mugabe katika nyadhifa za uwaziri na makamu wa rais. Yeye ndiye aliyefanya kazi ya kuondoa uchafu na kuuficha kwa niaba ya Mugabe.

Gazeti la Süddeutsche linasema Mnangagwa anataka kuleta mageuzi bila ya kugeuka na kuushughulikia uhalifu uliotendwa na kungwi wake - Mugabe na bila ya kondokana na itikadi za kizamani.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linazungumzia juu ya kifo cha Roy Bennett kilichosabishwa na ajali ya helikopta iliyotokea nchini Marekani. Gazeti hilo linasema kifo cha Roy Bennet, aliyekuwa mwasisi mmojawapo wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe, MDC, kinaongeza mtihani kwa wapinzani nchini humo. Marehemu huyo aliyekuwa mzungu, alisimama kidete kuupinga udikteta wa Mugabe.

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai(picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi)

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai

Roy Bennet amefariki wakati ambapo chama cha MDC hakimo katika hali nzuri. Kiongozi wake, Morgan Tsvangirai hana afya nzuri, na wakati  ambapo rais mpya Mnangagwa bado hajaonyesha dalili za kuleta  mabadiliko ya kweli.Gazeti hilo limemnukuu Tsvangirai akisema kuwa Roy Bennet ameacha pengo lisilozibika katika chama cha MDC.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Yusuf Saumu