Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 08.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

UJERUMANI

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yanazingatia juu ya kuporomoka kwa uchumi wa Kenya kutokana na mvutano wa kisiasa na pia shutuma za baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa Burundi.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine kuhusu hali ya nchini Kenya limemnukulu mtaalamu wa maswala ya kiuchumi wa Afrika Kusini akitahadharisha juu ya madhara yanayoweza kutokea katika uchumi wa Kenya katika kipindi cha muda mrefu kijacho.  Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine limemnukulu mtaalamu huyo Nick Charalambides wa kampuni ya ushauri inayoitwa Imani Development akisema kuwa wawekezaji wa vitega uchumi kutoka nje wanapata uhakika ikiwa nchi yenye utawala wa kisheria inaimarika.  Mtaalamu huyo alikuwa anajibu swali la mwandishi wa gazeti la Frankfurter Allgemeine kuhusiana na uamuzi wa mahakama ya juu nchini Kenya wa kuyabatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi uliopita. Muda mfupi baada ya uamuzi huo kutolewa hisa zilishuka thamani. Hata hivyo gazeti la Süd Deutsche Zeitung linamkariri kiongozi wa upinzani Raila Odinga akisema uamuzi wa mahakama umeonyesha njia mpya barani Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya bara hilo.

Gazeti la die tageszeitung wiki hii linatupia macho ripoti ya baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa juu ya hali ya nchini Burundi. Baraza hilo linadai kwamba utawala wa rais Pierre Nkurunziza umetenda uhalifu dhidi ya binadamu. Gazeti hilo linafahamisha. Katika ripoti ya uchunguzi wake tume iliyopewa jukumu la kufanya uchunguzi huo imetoa orodha ndefu ya madai juu ya utawala wa rais Nkurunziza.  Jambo jipya katika ripoti hiyo iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi mapema wiki hii ni ushahidi kwamba uhalifu dhidi ya binadamu ulitendeka nchini Burundi.  Orodha ya vitendo vya kihalifu ya tume hiyo inajumuisha mauaji ya kiholela, kamata kamata, watu kutoweshwa na ubakaji.

Gazeti hilo la die tageszeitung linaitaka mahakama ya kimataifa ICC ya mjini The Hague ianzishe hatua za kisheria dhidi ya utawala wa Pierre Nkurunziza. Gazeti hilo linaendelea kutufahamisha kuwa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa liliiunda tume hiyo ya kuchunguza hali ya nchini Burundi mnamo mwezi Septemba mwaka uliopita.  Hadi sasa tume kama hiyo ilishawahi kupelekwa nchini Eritrea, Korea Kaskazini na Syria. Hata hivyo gazeti hilo la die tageszeitung linaripoti kuwa wajumbe wa tume hiyo hawakuruhusiwa kuingia nchini Burundi ndio sababu ripoti ya tume hiyo imetokana na mahojiano waliyofanyiwa wakimbizi wa Burundi waliopo nje. Lakini serikali ya Burundi imekasirishwa na ripoti hiyo. Mshauri wa rais bwana Willy Nyamitwe amesema katika mtandao wa Twitter kwamba wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamefanya kazi kama mamluki. Gazeti hilo limemnukulu bwana Nyamitwe akisema wajumbe hao wamelipwa fedha na Umoja wa Ulaya ili kutoa taarifa zinazotokana na sababu za kisiasa.

Gazeti la Der Freitag wiki hii linatukumbusha juu ya jinamizi linaloendelea kuwasonga askari watoto wa Sudan Kusini. Gazeti hilo linasema wapo maelfu ya askari watoto nchini Sudan Kusini miongoni mwao David mwenye umri wa miaka 15.  Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa watoto zaidi ya elfu 18 waliandikishwa kuwa askari katika kipindi cha miaka minne iliyopita nchini Sudan Kusini. Mtoto mwingine James ambaye ana umri wa miaka 17 alilazimika kujiunga na kundi lililoitwa Cobra lililopambana na majeshi ya serikali. James alipoona maiti kwa mara ya kwanza alishtuka na wakati wote anaota juu ya kifo chake. Lakini gazeti hilo linasema kutokana juhudi za Umoja wa Mataifa askari watoto zaidi ya elfu moja na 900 wa Sudan Kusini walikombolewa kati ya mwaka 2015 na mwaka huu wa 2017.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Saumu Yusuf

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com