1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Albino walikuwa hatarini wakati wa uchaguzi , Tanzania

30 Oktoba 2015

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya jinsi walemavu wa ngozi nchini Tanzania wanavyotumiwa na wachawi.Pia yameandika juu ya ndovu wanaouliwa kwa sumu nchini Zimbabwe

https://p.dw.com/p/1GxM7
Albino walikuwamo hatarini wakati wa uchaguzi nchini Tanzania
Albino walikuwamo hatarini wakati wa uchaguzi nchini TanzaniaPicha: DW/P.Kwigize

Gazeti la "die tageszeitung" linakumbusha kwamba uchawi umepigwa marufuku nchini Tanzania, lakini wakati wa kampeni za uchaguzi uchawi ulipanda bei tena.

Ripota wa gazeti la "die tageszeitung" anaeleza kwamba watu wengi nchini Tanzania, pamoja na baadhi ya wanasiasa, wanaamini kwamba viungo vya mwili vya mtu mwenye ulemavu wa ngozi vinaleta kismati,yaani bahati njema.

Ripota wa "die tageszeitung" Ilona Eveleens anaeleza kuwa kuanzia mwaka wa 2000 watu 76 wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino wameuawa na wengine 46 walijeruhiwa vibaya kwa kukatwa miguu au mikono.

Katika kipindi hicho makaburi zaidi ya15 ya Albino yamefukuliwa na mabaki ya miili yaliibwa. Ndiyo sababu kwamba Albino wanaonekana kwa nadra katika mitaa nchini Tanzania.
Ripota wa "die tageszeitung" anaarifu kutoka Arusha,Tanzania kwamba wakati wa uchaguzi uchawi ulipanda bei tena, licha ya kupigwa marufuku na serikali.
Ripota huyo Ilona Eveleens amemnukulu mganga mmoja,Christian Kidanga mjini Arusha akisema kwamba wakati wa uchaguzi alikuwa anapata wateja hadi 15 kwa siku na hasa wanasiasa na watumishi wa serikali. Katika siku za kawaida "mganga" huyo hupata mtu mmoja au wawili tu.

Ripota wa gazeti la "die tageszeitung" amesema wanasiasa hao walienda kwa mganga huyo ili awapigie ramli kuhusu uchaguzi.

Jangwa la Sahara lawameza vijana wa Afrika

Gazeti la "Berliner wiki hii limeandika juu ya hatari inayowakabili wakimbizi wa Afrika wanaojaribu kulivuka jangwa la Sahara ili kufika barani Ulaya.

Gazeti hilo linasema wataalamu wanakadiria kwamba jangwa la Sahara linawameza wakimbizi sawa na jinsi wanavyomezwa na bahari ya Mediterania Vijana kutoka nchi kadhaa za Afrika wanaojaribu kukimbilia Ulaya wanapitia katika jangwa hilo.

Shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya uhamiaji , IOM limekaririwa na gazeti la "Berliner" likisema kwamba maiti 35 za vijana wa kiafrika zilikutwa zimeachwa katika malori mawili katika eneo moja la jangwa la Sahara.

Italien Flüchtlinge aus Eritrea fliegen nach Schweden Flughafen Ciampino
Wakimbizi kutoka Eritrea nchini ItaliaPicha: Reuters/R. Casilli

Na gazeti la "Süddeutsche" linatueleza kwa nini vijana wa kiafrika wanastahabu hatari hizo zote. Gazeti hilo linaizungumzia hali ya nchini Eritrea.

Linasema neno utumwa lina maana kubwa. Lakini jee vipi, vinginevyo, mtu ataweza kuilezea hali ya nchini Eritrea. Maalfu ya vijana wa Eritrea wanaondoka nchini ili kukwepa kulitumikia jeshi kwa mshahara usioweza kukidhi hata mahitaji ya lazima kwa muda wa wiki moja.


Gazeti la "Süddeutsche" linafahamisha kwamba mnamo mwaka wa 2013 vijana wapatao 22,000 waliomba hifadhi katika nchi mbalimbali duniani. Watu kutoka Eritrea wanahesabika kuwamo miongoni mwa wengi wanaopewa hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani.

Gazeti hilo linasema vijana wa Eritrea wanaikimbia nchi yao kwa sababu ya kulazimishwa kulitumikia jeshi kwa muda mrefu na kwa mshahara mdogo, hali inayofanana na utumwa.

Gazeti la "Berliner wiki hii pia limendika juu ya majangili waliotumia sumu kuwaua ndovu nchini Zimbabwe.

Gazeti hilo linafahamisha kwamba wanyama hao wanashikwa na maumivu makali na wanachukua muda mrefu kukata roho .Ikiwa ndovu hao wanaramba sehemu zilizotiwa sumu wanakunjika baada ya muda mfupi tu. Lakini kabla ya kufa inachukua muda mrefu wa kuteseka na maumivu makali.

Gazeti la "Berliner" linasema vifo vya ndovu vimeongozeka kwenye mbuga ya Hwange nchini Zimbabwe. Kuanzia mwezi wa Oktoba tembo 62 wameuliwa kwa kutiliwa sumu na majangili. Gazeti la Berliner limekumbusha kwamba mnamo mwaka wa 2013 tembo wapatao 300 waliangamizwa na majangili nchini Zimbabwe. Gazeti limearifu kuwa wahalifu wanawatilia sumu wanyama hao katika matunda, mahindi na katika maji.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu