Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 29.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na pia yamechapisha mahojiano na Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma

Hatari ya kutokea mauaji halaiki katika Jamhuri ya Afrika ya Kati

Hatari ya kutokea mauaji halaiki katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine" linasema katika taarifa yake kwamba kuna hatari ya kutokea mauaji ya halaiki katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwa sababu hakuna tena serikali katika nchi hiyo. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limearifu kwamba kutokana na hatari hiyo Ufaransa imeamua kuwapeleka askari wengine alfu moja katika nchi hiyo.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnukuu Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean Yves Le Drian akielezea sababu ya nchi yake kuichukua hatua hiyo.Waziri huyo amenukuliwa na gazeti hilo akisema kwamba kuna hatari ya kutokea mauaji halaiki katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Waziri Le Drian ameeleza kuwa nchi hiyo imo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na kwamba makundi yanayopingana yanauana.
Ufaransa tayari inao askari 450 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Watoto wa kiafrika wadhalilishwa

Gazeti la "Süddeutsche limeshchapisha makala juu ya malalamiko ya baadhi ya wanaharakati wa barani Ulaya juu ya jinsi watoto wa kiafrika wanavyoonyeshwa katika kamera ili kuchangisha fedha za misaada. Gazeti hilo linasema kwamba watoto wa kiafrika wanaonyeshwa wakiwa wanatoa macho makubwa,bila ya kusema lolote,mbele ya kamera. Gazeti hilo linaeleza kwamba hiyo ndiyo njia inayotumiwa na baadhi ya mashirika ya misaada katika kuchangisha fedha kutoka kwa watu barani Ulaya.

Gazeti "Süddeutsche"linatufahamisha kwamba mandhari hiyo imo katika tangazo la shirika la misaada kwa ajili ya watoto la "Child Fund International". Tangazo hilo linawaonyesha watoto wengi,wenye ukiwa,na wasiokuwa na sauti. Sauti inayosikika ni ile ya mzungu anaewataka watu watoe fedha.Gazeti la "Süddeutsche" linafahamisha kwamba tangazo hilo limeteuliwa kwa ajili ya kupewa tuzo ya "Rusty Radiator" Lakini gazeti hilo limearifu kuwa jopo la kimataifa limesema kwamba tangazo hilo, la shirika la misaada la "Child Fund International" linawadhalilisha watu ambao linakusudia kuwasaidia.

Nkosazana Dlamini-Zuma

Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii limechapisha mahojiano na Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini- Zuma. Katika mahojiano hayo Nkosazana Dlamini- Zuma ambae ni mwanamke wa kwanza barani Afrika kuuongoza Umoja wa Afrika amesema kwamba siyo sawa hata kidogo kwa Afrika kuwa masikini.

Mwanasiasa huyo ameliambia gazeti la "die tageszeitung"kwamba watu wa Afrika hawapaswi kujikunyata na kulalamika juu ya yale ambayo wengine wanayafanya duniani. Afrika haiwezi kuyabadilisha yanayofanywa na wengine,lakini inao uwezo wa kuyabadilisha inayoyafanya. Katika mahojiano hayo Nkosazana Dlamini- Zuma amesema, Afrika inapasa kujua kule inakotaka kuelekea. Ndiyo sababu haikubaliani kabisa na malengo ya Milenia. Kwa sababu lengo la mpango huo ni kupunguza umasikini kwa nusu hadi kufikia mwaka wa 2015 . Mwanasiasa huyo amesema haiwezekeni kuwaambia "watu wetu" kwamba ni sawa kuwa kuwa nusu masikini!

Ubunifu wa vijana wa Kenya
Gazeti la"Der Spiegel" limewafahamisha wasomaji wake kwamba utaratibu wa malipo unaoitwa MPesa ulioanzishwa na vijana wa Kenya, sasa unatumika katika takriban nchi zote zinazoendelea duniani.Gazeti hilo linatilia maanani kwamba ubunifu wa vijana wa Kenya unaliwezesha bara la Afrika kuliziba pengo la tekinolojia ya mtandao baina yake na sehemu nyingine za dunia.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu