Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 05.04.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya kuthibitishwa kwa Uhuru Kenyatta kuwa Rais wa Kenya licha ya mashtaka yanayomkabili kwenye Mahakama kuu ya Kimataifa ya mjini the Hague.

Rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta

Magazeti ya Ujerumani pia yameandika juu ya mkutano wa viongozi wa nchi za eneo la Afrika ya kati na Afrika Kusini uliofanyika mjini Djamena kuujadili mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya kati. Na gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema katika maoni yake kwamba ili kuleta utulivu nchini Mali, haitoshi tu kuwatimua waislamu wenye itikadi kali

Uhuru Kenyatta athibitishwa kuwa Rais:

. Gazeti la "die tageszeitung" limeandika juu ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya juu ya nchini Kenya kumthibitisha Uhuru Kenyatta kuwa Rais wa Kenya. Ripota wa gaezti hilo Ilona Eveleens amearifu kutoka Nairobi kwamba Kenyatta alikuwa tayari ameshashinda uchaguzi wa Rais kwa njia ya kura, lakini mshindi wa kweli ni Mahakama.

Mahakama ya Juu ya Kenya imesema uchaguzi ulikuwa wa haki na ulifanyika kwa njia ya uwazi. Pande zote zimeikubali hukumu ya Mahakama hiyo japo palitokea ghasia kidogo zilizofanywa na watu wanaomuunga mkono Raila Odinga aliepeleka malalamiko kwenye Mahakama hiyo.

Gazeti la"die tageszeitung" limeeleza katika taarifa yake kwamba kwa muda mrefu viongozi wa Kenya waliona ni jambo rahisi kumhonga hakimu,badala ya kuenda kwa wakili. Lakini tokea kuteuliwa kwa wakili wa haki za binadamu Willy Mutunga kuwa Jaji Mkuu, Jaji huyo ameutumia wadhifa wake na kupambana na ufisadi. Na tokea wakati huo,imani ya watu wa Kenya katika mfumo wa sheria imerejea.

Waujadili mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati:

Gazeti la "die tageszeeitung" pia limeandika juu ya mkutano wa viongozi wa eneo la Afrika ya Kati na Afrika Kusini kuujadili mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya kati.Gazeti hilo limeandika kwamba waliohudhuria mkutano huo katika mji mkuu wa Chad, Djamena walikuwa pamoja na Rais Jacob Zuma, wa Afrika Kusini, lakini waasi waliotwaa mamlaka katika Jamhuri ya Afrika ya kati hawakuwakilishwa moja kwa moja kwenye mkutano huo.


Wafungwa wa kisiasa waachiwa Sudan

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linayatupia macho matukio ya nchini Sudan. Limearifu juu ya kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa.Limeandika katika taarifa yake kuwa Rais Omar Bashir ametoa mwito wa kufanyika mdahalo baina ya wote na kwa ajili hiyo amewaachia huru wafungwa wa kisiasa saba jumanne iliyopita.Gazeti hilo limemnukuu Rais Bashir akisema,kwamba kuachiwa kwa wafungwa hao ni hatua ya kwanza ya kuhimiza mdahalo wa wote nchini Sudan. Hata hivyo gazeti la "Frankfuter Allgemeine" limesema haujulikani ni wafungwa wangapi wa kisiasa wamo katika jela za Sudan.

Gazeti la"Frankfurter Allgemeine" limefahamisha katika taarifa yake kwamba miongoni mwa wafungwa wa kisiasa waliochiwa jumanne iliyopita walikuwa Hisham Mufti na Abdel Aziz. Wapinzani hao maarufu walikamatwa kwa sababu tu ya kushiriki kwenye mkutano mjini Kampala baina ya wapinzani wa serikali ya Sudan na wawakilishi wa waasi wa majimbo ya Darfur na Blue Nile.

Mapigano yaendelea Mali

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" pia limeandika juu ya mgogoro wa nchini Mali.Linasema ili kuleta utulivu nchini humo haitoshi tu kuwatimua Waislamu wenye itikadi kali wanaoshirikiana na magaidi wa Al-Qaeda. Hatua zaidi zinalazimu kuchukuliwa. Mfumo mpya wa uongozi unahitajika nchini Mali.

Gazeti la "Neues Deutschland" pia limeandika juu ya Mali.Gazeti hilo linatilia maanani kwamba mapigano yamezuka upya katika mji wa Timbuktu, baada ya Ufaransa kutangaza kwamba itayaondoa majeshi yake kutoka Mali,hatua kwa hatua. Rais Francois Hollande amesema , kuanzia mwishoni mwa mwezi wa Aprili, Ufaransa itaanza kuwaondoa askari wake 4,000 nchini Mali.

Gazeti la "Neues Deutschland" limemkariri Rais Hollande akisema kuwa majeshi ya Ufaransa yamelifikia lengo lililokusudiwa: kwanza kuwazuia waasi kuingia katika mji mkuu Bamako, na pili kuwatimua wanaitikadi kali wa kiislamu na magaidi katika sehemu ya kaskazini mwa Mali,ambayo walikuwa wanaishikilia.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo