Zuma akiri ANC ilifanya makosa | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.12.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Zuma akiri ANC ilifanya makosa

Mwenyekiti wa chama tawala nchini Afrika Kusini, Jacob Zuma amekiri chama chake kilifanya makosa, ikiwa chama kipya cha siasa kilichojitenga na ANC cha Congress of the People, kimezinduliwa leo na kupata viongozi wake

Rais wa chama tawala cha African National Congress ANC, nchini Afrika Kusini, Jacob Zuma

Rais wa chama tawala cha African National Congress ANC, nchini Afrika Kusini, Jacob Zuma

Akihutubia mkutano wa wazee wa chama tawala cha African National Congress, ANC na waliokuwa katika jeshi la zamani chini ya utawala wa kibaguzi, Bwana Zuma amesema wamejifunza kutokana na makosa waliyoyafanya miaka 15 iliyopita.


Kauli hiyo ameitoa huku chama hicho kikiwa kinakabiliwa na kujiondoa kwa baadhi ya wajumbe wake wakuu ambao wamejiunga na chama cha Congress of the People(COPE), kitu ambacho wengi wanaona hiyo ni kama changamoto kwa ANC. Hata hivyo, Zuma amesema chama cha ANC kitaendelea kueneza ujumbe wa matumaini kwa maisha bora na kwamba ndicho chama pekee kinachoweza kuonyesha mshikamano wa kweli na usitawi wa nchi hiyo.


Wajumbe wa chama hicho cha COPE ambacho kimezinduliwa rasmi leo katika mji wa Bloemfontein, ambako pia ndiko kilipozaliwa chama cha ANC mwaka 1912, wamemchagua waziri wa zamani wa ulinzi wa Afrika Kusini, Mosiuoa Lekota kuwa rais wake. Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mkuu wa jimbo la Gauteng, Mbhazima Shilowa amechaguliwa kuwa makamu wa kwanza wa rais wa chama hicho, huku Lynda Odendaal akichaguliwa kuwa makamu wa pili.


Chama hicho cha COPE kimesema kitahakikisha kinakabiliana na masuala mbalimbali ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kupiga vita rushwa, umasikini, ukosefu wa ajira, vitendo vya kihalifu na kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Akizungumza mbele ya wajumbe 4,000 wa chama hicho mara baada ya kuchaguliwa Bwana Lekota amesema historia ya Afrika Kusini haitajirudia tena kwa kuwa chama hicho hakina misingi ya ubaguzi wa rangi, madaraja wala jinsia.


Lekota alikuwa waziri wa ulinzi kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka huu wa 2008 alipojiuzulu, akiwa ni miongoni mwa viongozi wa serikali na wajumbe wa juu wa ANC waliojiuzulu baada ya chama tawala kumtaka aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Thabo Mbeki kuachia madaraka, ambao pia ndio waanzilishi wa chama cha COPE. Aidha, Lekota aliwahi kuwa mfungwa wa kisiasa katika Kisiwa cha Robben, pamoja na waliokuwa vinara wa kupinga utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini kama Nelson Mandela.


Uzinduzi wa chama hicho umefanyika baada ya mkutano wa siku tatu uliokuwa ukizungumzia kuhusu masuala ya uongozi, kampeni za uchaguzi wa mwaka ujao, sera pamoja na katiba yake. Chama hicho kilichoanzishwa mara baada ya Mbeki kujiuzulu mwezi Septemba, mwaka huu, tayari kina wafuasi wapatao 500,000.
 • Tarehe 16.12.2008
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GHGo
 • Tarehe 16.12.2008
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GHGo
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com