Wakimbizi wa Kongo, Burundi waanza kurejea nyumbani
23 Aprili 2026
Hizo ni sauti za furaha za wakimbizi wa Kongo kutoka Burundipale walipouvuka mpaka wa Gatumba nchini Burundi na kuuvuka mpaka mwingine wa Kavimvira na kuingia mjini Uvira katika nchi yao ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na hivyo kuashiria hatua kubwa katika juhudi za kikanda za kuwezesha kurejea kwa hiari kwa watu waliokimbia makazi yao.
Wanaume, wanawake, na watoto hao, ambao walikuwa wamekimbia mashambulizi na machafuko ya silaha mashariki mwa Kongo wamerudi katika nchi yao baada ya miezi mitano waliyokaa katika nchi hiyo jirani. Claude Kashindi ni miongoni mwa wakimbizi hao, anaelezea furaha yake :
Kurejea huko kumeandaliwa kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na kwa ushirikiano na mamlaka za Kongo na Burundi. Walipofika Uvira, watu hao zaidi ya mia nne, ikiwa ni sehemu ya kwanza leo, walipokelewa katika vituo vilivyotengenezwa ili kuwapokea kwa muda kabla kurejea katika maisha yao ya kawaida.
Walakini, licha ya furaha ya kurejea nyumbani, wakongo hao bado wanaelezea wasiwasi mkubwa kutokana na ukosefu wa usalama unaoendelea katika vijiji vyao.
Mashirika ya kiraia yanakumbusha kwamba upatikanaji wa huduma za afya, elimu, ajira na kadhalika bado ni changamoto kubwa kwa watu hao ambao lazima wajenge upya kila kitu. Dunia Amisi ni Mratibu wa asasi ya kiraia iitwayo Machozi ya Raia, alisema ni vizuri kuwepo na mshikamano wa kijamii na wa kitaifa kwa raia hao wanaorejea nyumbani.
Gavana wa Kivu kusini chini ya utawala wa Kinshasa profesa Jean-Jacques Purusi amewasifu marais wa Kongo na Burundi kwa kuwarejesha wakongo hao nchini mwao, akihakikisha pia nia ya Kongo ya kurejesha amani ya kudumu mashariki.