Zimbabwe yatangaza kumalizika kwa mgao wa umeme
5 Julai 2023Serikali ya Zimbabwe imetangaza kumalizika kwa mgao mkubwa wa umeme ambao umeitikisa nchi hiyo kwa kuathiri shughuli za biashara na kuyaacha mamilioni ya makaazi bila nishati hiyo muhimu kwa hadi saa 19 kila siku.
Wizara ya Habari ya Zimbabwe imesema Baraza la Mawaziri la nchi hiyo limeridhishwa na tangazo la shirika la umeme la taifa la kumalizika kwa mgao wa umeme kufuatia hatua kadhaa ambazo zimechukuliwa na serikali.
Soma pia: Walimu na Madaktari wa Zimbabwe wagoma
Taarifa ya wizara hiyo haikufafanua hatua hizo zilizowezesha kusitishwa kwa mgao wa umme kwenye taifa hilo la kusini mwa Afrika ambalo kwa miaka mingi limekabiliwa na upungufu wa nishati hiyo. Hali ilikuwa mbaya zaidi mwaka jana pale kina cha maji kilipopungua kwenye bwawa kubwa la kufua umeme la Kariba linalotegemewa na nchi hiyo.
Hata hivyo tangazo la serikali lilitolewa hapo jana limepokelewa kwa hisia mseto na umma wa nchi hiyo ambapo baadhi wamesema bado hawapati huduma hiyo.