1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky aishukuru Ufilipino kuelekea mkutano wa amani

3 Juni 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemshukuru Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr kwa kukubali kuhudhuria mkutano ujao wa kilele utakaolenga kuvimaliza vita vya Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4gZXe
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.Picha: Nhac Nguyen/AFP/Getty Images

Kwenye ziara yake ya muda mfupi mjini Manila, baada ya kuhudhuria kongamano la usalama la Shangri-La huko Singapore, Zelensky amesema zaidi ya mataifa 100 yanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa amani utakaofanyika Juni 15 na 16, nchini Uswisi. 

"Tunahitaji sana msaada wa mataifa ya Asia. Tunaheshimu kila sauti, kila eneo, kila taifa lililoko kwenye kanda hii. Tunaitaka Asia itambue kinachotokea nchini Ukraine, ili itusaidie kuvimaliza vita, ni muhimu kwa viongozi wa Asia kuwepo kwenye mkutano wa kilele wa Amani," amesema Zelensky.

Zelensky amemwambia Marcos Jr kwamba kuhudhuria kwake kwenye mkutano huo kutatoa ishara thabiti na hatua madhubuti kuelekea amani.

Ukraine pia imetangaza kuufungua ubalozi wake mjini Manila.