1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy akubali kuachana na azma ya kujiunga na NATO

Iddi Ssessanga rtre,afpe,ape
14 Desemba 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema kwenye mkutano wa Berlin kuwa yuko tayari kuachana na azma ya kujiunga na NATO kwa dhamana za usalama, lakini amekataa shinikizo la Marekani la kuitaka Ukraine kuachia ardhi.

https://p.dw.com/p/55KjR
Ukraine, Kyiv 2025 | Volodymyr Zelenskyy ampokea Nikos Christodoulides mjini Kyiv
Rais Volodymyr Zelenskiy amesema yuko tayari kuachana na azma ya kujiunga na jumuiya ya NATO lakini siyo kuachia ardhi yake kwa UrusiPicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema yuko tayari kuachana na azma ya nchi yake kujiunga na muungano wa kijeshi wa NATO. Alisema hatua hiyo inaweza kufanyika iwapo Ukraine itapewa dhamana madhubuti za usalama kutoka kwa washirika wa Magharibi.

Zelenskiy alitoa kauli hiyo Jumapili alipokutana na wajumbe wa Marekani wanaohusika na juhudi za kumaliza vita. Mazungumzo hayo yalifanyika huku Marekani ikiongeza shinikizo la kufikia makubaliano ya haraka ya kusitisha mapigano.

Katika mkutano huo, Zelenskiy alikutana na mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff. Pia alishiriki mazungumzo na Jared Kushner, mkwe wa Rais Trump.

Rais wa Ukraine alionekana katika picha akikaa mezani na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz. Wajumbe wa Marekani walikaa upande wa pili wa meza ya mazungumzo.

Ujerumani, Berlin 2025 | Mwanzo wa mazungumzo ya Ukraine yakimshirikisha Zelenskyy, Merz na Witkoff
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akimkaribisha mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff, Kansela Friedrich Merz akiwa pembeni, kabla ya mazungumzo ya Berlin kuhusu usitishaji mapigano.Picha: Guido Bergmann/Bundesregierung/dpa/picture alliance

Akijibu maswali ya waandishi wa habari kabla ya mazungumzo, Zelenskiy alisema kuwa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zilikuwa zimekataa ombi la Ukraine kujiunga na NATO. Hivyo, Kyiv sasa inatarajia aina nyingine ya ulinzi wa usalama.

Mkwamo wa ardhi na dhamana za usalama

Zelenskiy alisema dhamana hizo za usalama zinapaswa kufanana na zile zinazotolewa kwa nchi wanachama wa NATO. Alisisitiza kuwa dhamana hizo ni muhimu kuzuia wimbi jipya la uchokozi kutoka Urusi.

Alisema dhamana hizo lazima ziwe na nguvu ya kisheria na ziidhinishwe na Bunge la Marekani. Zelenskiy aliongeza kuwa anatarajia taarifa zaidi baada ya mkutano wa maafisa wa kijeshi wa Ukraine na Marekani nchini Ujerumani.

Urusi imekuwa ikipinga vikali azma ya Ukraine kujiunga na NATO. Rais Vladimir Putin ameitaja kama tishio kubwa kwa usalama wa Moscow na sababu ya kuivamia Ukraine mwaka 2022.

NATO ni nini?

Kremlin imedai Ukraine iachane kabisa na azma ya NATO kama sharti la makubaliano yoyote ya amani. Kyiv imekataa sharti hilo bila dhamana mbadala za usalama.

Zelenskiy pia alikataa pendekezo la Marekani la Ukraine kujiondoa katika eneo la Donetsk. Alisema pendekezo la kuanzisha eneo lisilo na wanajeshi na la kiuchumi huru halitekelezeki.

Mashambulizi ya anga yaendelea pande zote

Rais wa Ukraine alisema suala la ardhi ni nyeti sana kwa nchi yake. Alisisitiza kuwa chaguo la haki zaidi ni kusimamisha mapigano kulingana na mstari wa sasa wa mawasiliano.

Urusi, kwa upande wake, imesema haitawaondoa maafisa wake wa usalama katika maeneo ya Donetsk hata kama yatatangazwa kuwa yasiyo na wanajeshi. Kauli hiyo ilitolewa na mshauri wa masuala ya kigeni wa Putin, Yuri Ushakov.

Ushakov alionya kuwa juhudi za kufikia muafaka zinaweza kuchukua muda mrefu. Alisema mapendekezo ya Marekani yamebadilishwa vibaya na Ukraine pamoja na washirika wake wa Ulaya.

Urusi, Moscow 2025 | Mazungumzo ya washauri wa marais wakati wa mazungumzo kati ya Putin na Tokayev
Mshauri wa masuala ya kigeni wa Rais Vladmir Putin, Yuri Ushakov.Picha: Roman Naumov/Picvario Media/picture alliance

Wakati huo huo, mashambulizi ya anga yameendelea kati ya pande hizo mbili. Jeshi la anga la Ukraine lilisema Urusi ilirusha makombora na droni zaidi ya 130 usiku mmoja.

Zelenskyy alisema mashambulizi hayo yamewaacha mamia ya maelfu ya raia bila umeme katika maeneo kadhaa. Aliongeza kuwa Urusi imeongeza mashambulizi ya droni na makombora katika wiki za hivi karibuni.