1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenksy aishtumu Urusi kwa kufanya mauaji ya halaiki

27 Mei 2022

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine ameyatolea mwito mataifa ya magharibi kuipa Kyiv silaha zaidi wakati Rais Volodymyr Zelenksy akiishtumu Moscow kwa kufanya mauaji ya halaiki katika eneo la mashariki la Donbas.

https://p.dw.com/p/4Bxnu
Ukraine, Präsident Selenskyj
Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Katika ujumbe aliouandika kupitia ukurusa wake wa Twitter, Waziri Dmytro Kuleba amesema Ukraine inahitaji silaha nzito akisema, bila ya silaha hizo haitokuwa rahisi kupambana na vikosi vya Urusi ambavyo vinaonekana kuwa na silaha za kisasa.

Waziri huyo ameongeza kuwa hali katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambamo vikosi vya Urusi vimezidisha mashambulizi, ni mbaya mno.

Soma pia:Urusi yaelekeza mashambulizi yake mkoa wa Donbas 

Amesema, "Kwa kweli hali ni mbaya zaidi hata kuliko watu wanavyosema. Tunahitaji silaha. Iwapo kweli munaijali Ukraine, tunahitaji silaha.” 

Wakati hayo yanaripotiwa, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksy ameishtumu Urusi kwa kutekeleza kile alichokiita mauaji ya halaiki katika eneo la mashariki la Donbas.

Katika hotuba yake ya kila siku ya kutafuta uungwaji mkono, Zelensky amelaani mashambulizi ya kikatili katika eneo la Donbas- sehemu ambayo Urusi imelekeza nguvu zake zote baada ya kushindwa kuutia mikononi mwake mji mkuu wa Kyiv.

Zelenksy ameongeza kuwa mashambulizi ya Urusi yanaweza kuliacha eneo hilo bila wakaazi wowote. Amesema, "Hali mbaya ya maafa inayotokea ingeweza kusitishwa iwapo dunia ingeichukulia hali ya Ukraine kama yao wenyewe. Iwapo mataifa yenye nguvu duniani yangesimama wima dhidi ya Urusi na kuishinikiza kumaliza vita."

Makundi yanayotaka kujitenga na yanayoungwa mkono na Urusi tangu mwaka 2014 yamedhibiti sehemu kadha za Donbas, japo kutokana na mashambulizi ya sasa, inaonekana kuwa Urusi inataka kulichukua kabisa eneo lote.

Wanajeshi wa Urusi wameuzingira mji wa Sievierodonetsk

Ukraine Brücke nach Severodonetsk
Daraja linalounganisha mji wa Lysychansk na Severodonetsk mashariki mwa eneo la Donbas limeharibiwaPicha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Gavana wa jimbo la Luhansk Serhiy Haidai amesema watu wanne wameuawa katika mji wa mashariki wa Sievierodonetsk katika muda wa saa 24 zilizopita. Gavana huyo ameongeza kuwa, mtu mwengine aliuawawa katika shambulio la Urusi katika Kijiji cha Komushuvakha.

Katika ujumbe aliouandika katika mtandao wa Telegram leo Ijumaa, gavana Haidai amesema wakaazi wa mji wa Sievierodonetsk wanaishi kwa hofu kutokana na mashambulizi yasiokwisha ya vikosi vya Urusi.

Soma pia:Ukraine lazima iamue mustakabali wake yenyewe: Duda 

Kauli yake imeungwa mkono na meya wa mji huo Oleksandr Stryuk aliyesema kuwa karibu asilimia 60 ya majengo katika mji huo yameharibiwa.

Kulingana na takwimu za mamlaka nchini Ukraine, watu wapatao 1,500 wameuawa katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kulikoshuhudiwa mapambano makali tangu kuanza kwa vita hivyo.

Meya Stryuk amesema miongoni mwa waliopoteza maisha ni wanajeshi na raia wa kawaida na kwamba idadi kubwa ya wakaazi wa mji Sievierodonetsk wamekimbia. Asilimia 10 tu ya takriban wakaazi 130,000 waliokuwa wakiishi mjini humo ndio waliosalia.