1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen: watu kadhaa wauawa katika shambulio la hospitali

Yusra Buwayhid
7 Novemba 2019

Madaktari Wasio na Mipaka wasema watu wanane wameuawa, katika mji wa bandari wa al-Makha, baada ya hospitali yao kushambuliwa magharibi mwa Yemen.

https://p.dw.com/p/3SbpO
Karte Jemen Saada EN

Shambulio hilo lilofanywa kwa ndege isiyokuwa na rubani pamoja na kombora limelenga majengo karibu na hospitalini, na kusababisha milipuko mikubwa na vifo vya watu wasiopungua wanane.

Taarifa ya Madaktari Wasio na Mipaka imesema imeifunga hospitali hiyo kwa sababu ya shambulio lilotokea.

Taarifa hiyo imeongeza kwamba hakuna ripoti za vifo au majeraha kati ya wagonjwa wake. Walihamishwa kwenda katika vituo vingine vya afya katika Mji wa Bahari ya Sham wa al-Makha ambao unajulikana pia kama Mocha.

Wadah Dobish msemaji wa serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, amesema waasi wa Houthi wameshambulia maghala yanayotumiwa na vikosi vinavyashirikiana na serikali Jumatano usiku na kusababisha moto mkubwa.

Soma zaidi:Wahouthi wadai kuteka maelfu ya wanajeshi wa Saudi Arabia

Shirika la Madktari Wasio na Mipaka ambalo pia linajulikana kama MSF limesema hospitali hiyo ilifunguliwa Agosti mwaka jana, na inatoa huduma za bure kwa watu waliojeruhiwa kwa vita pamoja na huduma ya upasuaji.

Yemen bado imegawanyika

Hospitali ya Mocha kimsingi ndio kituo pekee kinachotoa huduma kwa maelfu ya watoto walio na utapiamlo mbaya. Kinahudumia watu wa Mocha au jamii za watu waliokimbilia Mocha zaidi ya mwaka mmoja uliopita wakikimbia mapigano katika maeneo mengine.

Humanitäre Krise in Jemen
Mtoto aliye matatizo ya lishe kwa sababu ya ukosefu wa chakula nchini YemenPicha: picture-alliance/M. Hamoud

Abdel-Rahman Ahmed, daktari katika hospitali hiyo, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba: "wagonjwa walikimbia baada ya mlipuko mkubwa kutokea, kufuatia shambulio la kombora dhidi ya ghala ya silaha kulitikisa eneo hilo."

Soma zaidi: Serikali ya Yemen na waasi watia saini makubaliano ya amani

Baada ya miaka mitano ya mgogoro, Yemen bado ni nchi iliygawanyika. Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wamekuwa wakiudhibiti mji mkuu wa Sanaa pamoja na maeneo mengine ya kaskazini mwa nchi tangu mwaka 2014.

Huku muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na kuungwa mkono na Marekani ukielemea upande wa serikali ya Rais Abed Rabbo Mansour Hadi.

Muungano huo wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia ulianza kampeni yake ya mashambulizi ya anga mnamo mwaka 2015.

Kulingana na shirika linalofuatilia migogoro la ACLED mashambulizi ya angani na ardhini yamesababsiha vifo vya watu 100,000 ikiwa ni raia wa kawaida pamoja na wapiganaji. Vita vile vile vimesababisha hali ya njaa katika maeneo mengine nchi humo.

ap