YANGON : Jeshi laonya kuwapiga risasi waandamanaji | Habari za Ulimwengu | DW | 27.09.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

YANGON : Jeshi laonya kuwapiga risasi waandamanaji

Umma wa waandamanaji katikati ya mji mkuu wa Yangon umetawanyika leo hii baada ya wanajeshi zaidi ya 200 na polisi kuingia mitaani na vipaza sauti wakiwaamuru watu kurudi nyumbani venginevyo watakuwa katika hatari ya kuuwawa kwa kupigwa risasi.

Mapema mtu mmoja alianguka baada ya kufyatuliwa risasi na haikuweza kufahamika mara moja iwapo alikuwa amekufa au la.

Habari kutoka Burma zinasema vikosi vya usalama vimevamia nyumba kadhaa za watawa wa kibuda na kuwatia mbaroni watawa 200 wanaotuhumiwa kuratibu maandamano makubwa kuwahi kushududiwa nchini humo katika kipindi cha miaka 20.Vizuizi pia vimewekwa katika vituo muhimu kwenye mji mkuu wa nchi hiyo kwa lengo la kuzuwiya maandamano mapya dhidi ya serikali.

Hapo jana vikosi vya usalama vya nchi hiyo viliwauwa kwa kuwapiga risasi takriban wanaharakati watano na kuwatia mbaroni mamia ya watu.

Mataifa ya magharibi yamelaani matumizi ya nguvu ya watawala wa kijeshi wa Burma na yametowa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufikiria kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

Umoja wa Ulaya na Marekani zimetowa taarifa ya pamoja kuitaka serikali ya Burma kukomesha matumizi ya nguvu na kuanza mazungumzo na viongozi wanaotetea demokrasia akiwemo Aung San Suu Kyi.

Thomas Steg naibu msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema hata katika kikao cha baraza la mawaziri Kansela wa Ujerumani amesisitiza kwa mara nyengine tena kwamba anategemea kutoka kwa viongozi wa Burma kwamba hawatotumia nguvu na watafunguwa njia kuelekea demokrasia na amani.

Wakati huo huo balozi wa China kwenye Umoja wa Mataifa amesema kwamba vikwazo dhidi ya Burma havitosaidia.

Nchi jirani ya India imetowa wito wa kufanyika kwa mageuzi ya kisiasa nchini humo.

Jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na kikao cha dharura juu ya Burma.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com