1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wengi wanaishi katika maeneo yaliyodhoofika, ripoti

19 Septemba 2025

Ripoti mpya ya Benki ya Dunia imebainisha kuwa 90% ya watu duniani wanaishi katika maeneo ya ardhi iliyodhoofika, maji na hewa chafu.

https://p.dw.com/p/50lq0
Skyline Nairobi
Kenya imezindua hivi karibuni vifaa vya aina yake vya kupima viwango vya ubora wa hewa jijini Nairobi.Picha: Thomas Imo/picture alliance/photothek

Kulingana na ripoti hiyo matumizi sahihi ya mazingira yanaweza kupunguza uharibifu wa mazingira kwa nusu. Kwa Kenya, tathmini hiyo inatolewa wakati ambapo imezindua mashine mpya za kupima viwango vya uchafuzi wa hewakatika mji wake mkuu. 

Ripoti hiyo mpya ya Benki ya Dunia inatahadharisha kuwa uharibifu wa mazingira unaathiri ukuaji wa uchumi na maendeleo ya binadamu kwa kiasi kikubwa. Tathmini hiyo inabainisha kuwa watu wanane kati ya kumi walioko kwenye mataifa masikini wanakabiliana na ukosefu wa hewa safi, maji safi na ardhi yenye rutba. Ripoti inasisitiza kuwa iwapo mazingira yanalindwa na kutumika vizuri yanaweza kuwa chachu ya maendeleo na kutoa nguvu ya kuhimili mabadiliko.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu Axel Trotsenburg wa ngazi ya juu anayehusika na sera ya maendeleo ya ulimwengu na ushirikiano katika Benki ya Dunia, ripoti hiyo inatoa nafasi ya kutazama changamoto hizo za mazingira kwa jicho la fursa ya kusaka suluhu za kisasa za maendeleo.

Kenya Nairobi | Changamoto ya uchafuzi wa mazingira
Ripoti ya Benki ya Dunia inatoa nafasi ya kutazama changamoto hizo za mazingira kwa jicho la fursa ya kusaka suluhu za kisasa za maendeleo.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kauli hizo zimetolewa wakati Kenya imezindua hivi karibuni vifaa vya aina yake vya kupima viwango vya ubora wa hewa jijini Nairobi. Akizungumza kwenye uzinduzi wa vifaa hivyo vya kupima ubora wa hewa, Waziri wa Mazingira katika serikali ya kaunti ya Nairobi, Geoffrey Mosiria aliusisitizia umuhimu wa kuleta uwiano kati ya sera na utendaji wa kazi ili kupambana na uchafuzi wa mazingira. Maurice Kavai, Naibu Mkurugenzi wa Mabadiliko ya tabia nchi na uangalizi wa ubora wa hewa katika kaunti ya Nairobi, anashikilia kuwa kila mkaazi wa jijini anawajibika kuufanikisha mradi huo.

Ifahamike kuwa serikali ya kaunti ya Nairobi ilizindua jumla ya vifaa 50 vya bei nafuu vya kupima ubora wa hewa kwenye maeneo bunge 17 chini ya mpango wa Breathe Nairobi. Vifaa vyengine 39 tayari vilikuwa vinaendelea na kazi tangu katika awamu ya majaribio. Seneca Vieira, msimamizi wa kiufundi katika mpango wa Breathe Cities Africa aliyehudhuria uzinduzi wa vifaa hivyo vya kupima ubora wa hewa, alifafanua kuwa matokeo yake yatawapa muongozo muhimu utakaoishirikisha jamii na pia wataalam ili kuandaa miradi ya kuimarisha hewa katika miji miengine barani Afrika.

Juhudi za kukabili uchafuzi wa hewa mjini Nairobi
Juhudi za kukabili uchafuzi wa hewa mjini NairobiPicha: DW

Nairobi ilijiunga na mpango wa Breathe Cities Initiative Septemba mwaka 2024, unaoshirikisha wakfu wa Clean Air Fund, C40 Cities na Bloomberg Philanthropies. Mradi una azma ya kuimarisha ubora wa hewa, kupunguza gesi za kaboni na kuimarisha pia afya ya umma kote ulimwenguni. Ifahamike kuwa kwa sasa takwimu za serikali ya kaunti zinaashiria kuwa asilimia 10 ya bajeti yake ya mwaka imetengewa tiba ya magonjwa yanayosababishwa na hewa chafu. Pamela Ejera ni mkaazi wa mtaa wa Mathare ambao uko karibu na jaa la taka la Dandora. Moshi wa magari na hewa chafu vimemsababishia kupata magonjwa ya macho.

Jiji la Nairobi ni moja ya 14 yanayoshiriki kwenye mpango wa kudumisha hewa safi kote ulimwenguni. Mikakati kama hii inashabihiana na mapendekezo ya ripoti hiyo ya Benki ya Dunia ya kusaka suluhu za kisasa ili kulinda mazingira. Ripoti yenyewe inasisitiza kuwa uchafuzi wa hewa na maji unavuruga utendaji wa kazi, mitazamo na kumaliza nguvu uwezo wa binadamu.