Wanaharakati wasema watu wasiopungua 6,126 wameua Iran
27 Januari 2026
Madai hayo yametolewa wakati msafara wa meli za kivita za Marekani ukiwasili Mashariki ya Kati, hatua iliyoongeza hofu ya uwezekano wa Marekani kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran. Mataifa ya Ghuba, kwa upande wao, yameeleza kuwa hayatahusika moja kwa moja na shambulio lolote, licha ya kuendelea kuwahifadhi wanajeshi wa Marekani katika maeneo yao.
Kuwasili kwa manowari ya kubeba ndege za kivita ya USS Abraham Lincoln, pamoja na meli za kivita za kuharibu makombora zinazoisindikiza, kunaongeza uwezo wa kijeshi wa Marekani katika eneo hilo. Hatua hii imekuja huku mataifa ya Kiarabu ya Ghuba yakisisitiza kuwa hayana nia ya kushiriki katika shambulio lolote dhidi ya Iran, licha ya ushirikiano wao wa kijeshi na Washington.
Makundi mawili ya wanamgambo wanaodaiwa kuungwa mkono na Iran katika Mashariki ya Kati yameonyesha utayari wa kufanya mashambulizi mapya. Hatua hii inaelezwa na wachambuzi kama jaribio la kuashiria mshikamano na Iran, baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutishia kuchukua hatua za kijeshi kufuatia madai ya mauaji ya waandamanaji au ukandamizaji wa maandamano nchini Iran.
Iran imekuwa ikitishia mara kwa mara kuwa mzozo wowote mkubwa unaweza kuhusisha Mashariki ya Kati nzima. Hata hivyo, wachambuzi wanasema uwezo wake wa kijeshi, hususan ulinzi wa anga, umepata pigo kufuatia mapigano ya Juni yaliyoihusisha na Israel.
Wakati huohuo, nchi hiyo inakabiliwa na shinikizo kubwa la kiuchumi. Uhaba wa bidhaa za matumizi ya kila siku umeongezeka, huku sarafu ya Iran, rial, ikishuka hadi kiwango cha chini kabisa kuwahi kurekodiwa — takribani rial milioni 1.5 kwa dola moja ya Marekani.
Takwimu za vifo na ukamataji
Shirika la Human Rights Activists News Agency lenye makao yake Marekani limetoa takwimu mpya, likidai kuwa watu 5,777 waliuawa wakati wa machafuko ya hivi karibuni. Kwa mujibu wa shirika hilo, waliouawa ni pamoja na waandamanaji, wanajeshi na vikosi vya serikali, watoto, pamoja na raia ambao hawakuhusika na maandamano. Zaidi ya watu 41,800 wanadaiwa kukamatwa.
Hata hivyo, Shirika la Habari la Associated Press limesema halijaweza kuthibitisha idadi hiyo kwa njia huru, kutokana na mamlaka za Iran kukata huduma ya intaneti na kuvuruga mawasiliano ya simu. Serikali ya Iran, kwa upande wake, imetoa takwimu ndogo zaidi za vifo, ikisema waliouawa walikuwa 3,117, wengi wao wakiwa raia na maafisa wa usalama, huku wengine wakitambuliwa kama "magaidi”.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amekosoa kusogezwa kwa meli za kivita za Marekani, akisema hatua hiyo haitadhoofisha nia wala azma ya Iran.
"Tuna dhamira thabiti pamoja na uwezo kamili wa kuilinda Iran. Ni wazi kabisa jinsi tutakavyojibu. Kama tulivyothibitisha hapo awali, mbele ya uchokozi wowote au tishio lolote, tutajibu kwa uamuzi, kwa nguvu kamili na kwa njia ya kina,” alisema Baghaei.
Lawama za nje na ‘mhimili wa upinzani'
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeendelea kuwalaumu majeshi ya nje kwa kuchochea maandamano. Wakati huohuo, utawala wa kidini nchini humo unaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi, huku vikwazo vya kimataifa — hususan vinavyohusiana na mpango wa nyuklia — vikiendelea kuibana nchi hiyo.
Iran pia imekuwa ikionyesha ushawishi wake wa kikanda kupitia mtandao unaoitwa "Mhimili wa Upinzani”, unaojumuisha makundi washirika katika Gaza, Lebanon, Yemen, Syria na Iraq. Mtandao huo hutajwa na Tehran kama ngao ya kuzuia migogoro kufika ndani ya mipaka yake.
Katika hatua mpya, Umoja wa Ulaya umetangaza nia ya kuwawekea vikwazo maafisa wakuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC). Wanadiplomasia wamesema hatua hiyo itahusisha kufungiwa mali na marufuku ya kusafiri kwa watu na taasisi 21, wakiwemo maafisa wa ngazi za juu wa IRGC.
Uamuzi huo unatarajiwa kuidhinishwa na mabalozi wa nchi wanachama kabla ya kupitishwa rasmi na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya watakapokutana mjini Brussels.
Chanzo: Mashirika