1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kadhaa wauliwa katika shambulio la bomu harusini

Sekione Kitojo
18 Agosti 2019

Mripuko wa shambulio la  bomu  la  kujitoa  muhanga ulitokea katika sherehe  ya  harusi  usiku  wa  Jumamosi  katika mji mkuu Afghanistan na watu kadhaa  waliuwawa  ama  kujeruhiwa, amesema afisa wa  serikali.

https://p.dw.com/p/3O4rI
Afghanistan Explosion bei Hochzeitsfeier in Kabul
Picha: Reuters/M. Ismail

Zaidi  ya  watu 1,000 walialikwa, amesema  mtu  mmoja aliyeshuhudia, wakati  hofu  ikitanda  kuwa  inaweza  kuwa shambulio  baya  kabisa  kuwahi  kutokea  mjini Kabul mwaka  huu.

Afghanistan Explosion bei Hochzeitsfeier in Kabul
Baadhi ya majeruhi katika hospitali mjini Kabul baada ya mripuko wa bomu katika harusiPicha: Reuters/M. Ismail

Msemaji  wa  wizara  ya  mambo  ya  ndani Nusrat Rahimi ameliambia  shirika  la  habari  la  Associated Press kuwa mshambuliaji  alijiripua  miongoni mwa  washiriki  wa  sherehe  hiyo ya  harusi. Kundi  la  Taliban  na  washirika  wake  wa  ndani  wa kundi  linalojiita  Dola  la  Kiislamu  hufanya  mashambulizi  ya umwagaji  damu  katika  mji  mkuu  huo.

Mripuko  huo  ulitokea  karibu  na  jukwaa  ambako  wanamuziki walikuwa  na "vijana  wote , watoto  na  watu  wote ambao  walikuwa katika  eneo  hilo  waliuwawa," mtu  aliyeshuhudia  Gul Mohammad alisema. Mmoja  kati  ya  waliojeruhiwa , Mohammad Toofan, alisema kwamba "wageni  wengi waliuwawa."

Maafisa  hawakutarajiwa  kutoa idadi yoyote  ya  waliofariki  hadi leo  Jumapili (18.08.2019).

Miili ya watu imetapakaa ukumbini

"Kuna  watu  wengi  waliofariki na  kujeruhiwa,"  alisema  Ahmad Omid, aliyenusurika ambaye  alisema  kiasi wageni 1,200 walialikwa katika  harusi  hiyo ya  mpwa wa baba  yake. "Nilikuwa  na bwana harusi katika  chumba  kingine  ambako tulisikia mripuko huo na kisha  sikuweza  kumpata mtu yeyote. Kila  mtu alikuwa  amelala chini katika  ukumbi  huo."

Afghanistan Selbstmordanschlag auf Hochzeit SYMBOLBILD
Wauguzi wakimhudumia majeruhi katika shambulio la bomu mjini Kabul katika sherehe ya harusiPicha: AP

Nje  ya  hospitali mjini  humo, wana  familia  walikuwa  wakilia. Wengine walitapakaa  damu.

Mripuko  huo  katika  ukumbi  wa  harusi  wa  dubai City magharibi mwa  Kabul, sehemu ya  mji  huo  ambayo  wanaishi,  wengi  ni watu wa kabila  la  wachache  wa  jamii  ya  washiia  wa  Hazara, walifikisha  mwisho kipindi  cha  utulivu.

Agosti 7 , shambulio  la  bomu  lililokuwa  katika  gari  lililofanywa  na kundi  la  Taliban lililolenga  vikosi  vya majeshi  ya  usalama ya Afghanistan liliripuka katika  barabara  hiyo hiyo, na  kuwauwa watu 14 na  wengine 145 walijeruhiwa, wengi  wao  wakiwa  wanawake, watoto na  raia  wengine.

Afghanistan Tote nach Explosion bei Hochzeitsfeier in Kabul
Polisi wa Afghanistan wakilinda jengo la ukumbi wa harusi mjini Kabul lililoshambuliwa kwa mripuko wa bomu la kujitoa muhangaPicha: AFP/R. Maqbool

Kumbi  kubwa za  harusi mjini  Kabul zilizopambwa  vizuri  na  kuwa na  taa  nyingi ni vituo vya  maisha  ya  jamii  katika  mji huo unaoandamwa  na  vita  kwa  miongo  kadhaa, ambapo  maelfu ya dola  hutumika katika  usiku  mmoja.

"Tumefadhaishwa  na  taarifa  za  shambulio  la  kujitoa  muhanga katika  ukumbi  wa  harusi  mjini  Kabul. Uhalifu wa kiwoga  dhidi ya watu  wetu; inawezekana  vipi  kumfunza  binadamu  na  kumwambia aende  kujiripua  ndani ya  harusi ? !! Sediq Seddiqi, msemaji wa rais Ashraf Ghani, amesema  katika  maandishi  katika  ukurasa wa Twitter.