Watu 85 wauawa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel
19 Septemba 2025
Aidha Israel imeendeleza operesheni yake ya kijeshi katika jiji la Gaza huku maelfu ya Wapalestina wakiendelea kuondoka katika jiji hilo. Mashambulizi hayo yamepelekea kukatika kwa umeme na mawasiliano ya simu na intaneti.
Hayo yakiarifiwa, Marekani kwa mara nyingine tena imetumia kura yake ya turufu hapo jana Alhamisi na kuzuia kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotaka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza , kuwezesha ufikiaji wa misaada ya kibinadamu na kuachiliwa kwa mateka.
Azimio hilo liliungwa mkono na wanachama wote 14 wa baraza hilo ispokuwa Marekani ambayo ilipendekeza uwepo wa azimio la kibinaadamu pekee. Lakini Ufaransa, Uingereza na Urusi zilitilia shaka faida na ufanisi wa azimio la kibinadamu pekee kutoka kwa chombo kilichoundwa kwa ajili ya kudumisha amani na usalama duniani.