Watu 3 wauwawa kwa guruneti Mombasa | Matukio ya Afrika | DW | 04.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Watu 3 wauwawa kwa guruneti Mombasa

Watu 3 wameuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa Jumamosi (03.05.2014) wakati milipuko miwili ilipotokea katika mji wa bandari wa Mombasa katika pwani ya Kenya. Hayo ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo.

Mkuu wa jeshi la polisi mjini Mombasa, Robert Kitur, ameliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA, kwa njia ya simu kwamba watu wote watatu walikufa wakati guruneti liliporushwa kwenye kituo cha basi cha Mwembe Tayari katikati mwa jiji la Mombasa mwendo wa saa 2.15 usiku. Hata hivyo Kitur hakutoa maelezo zaidi. Shirika la msalaba mwekundu limeripoti watu 21 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo.

"Kilichotokea ni kwamba guruneti limevurumishwa kwa abiria," amesema kamishna wa kaunti ya Mombasa, Nelson Marwa, wakati alipozungumza na waandishi wa habari. "Washambuliaji walikuwa wakiendesha pikipiki, na kulirusha guruneti hilo kwenye umati wa watu waliokuwa katika kituo cha basi."

Katika kituo hicho cha basi wahanga wa shambulizi hilo walionekana wakiwa chini katika kidimbwi cha damu na barabara ilikuwa imejaa vipande vya glasi kutoka kwa madirisha ya basi yaliyovunjika. "Sikuona aliyerusha kitu hicho, lakini nilisikia mlipuko mkubwa kabla kuanguka chini. Baadaye nilihisi miguu yangu inapoteza hisia," amesema Halima Sidi mwenye umri wa miaka 26, anayefanya kazi katika duka moja la bidhaa, alipozungumza na shirika la habari la Reuters katika hospitali moja wakati wauguzi walipokuwa wakiufunga bendeji mguu wake ulioumia.

Bombenanschläge in Mombasa Kenia 3.5.14

Basi lililoharibiwa katika shambulizi la Mombasa

Shambulizi la Nyali

Mkuu wa jeshi la polisi mjini Mombasa, Robert Kitur, amesema mlipuko wa pili umetokea katika hoteli ya Reef katika kitongoji cha Nyali, kaskazini mwa Mombasa, lakini hakuna yeyote aliyejeruhiwa. Walinzi katika hoteli hiyo wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba walifaulu kuwazuia washambuliaji kuingia katika hoteli hiyo, lakini wakarusha mkoba uliokuwa na kilipuzi katika kiwanja cha hoteli hiyo. Dari la mojawapo ya majengo limeharibiwa kabisa na mlipuko uliotokea na sehemu ya ukuta wa jengo hilo umeanguka.

Ranjit Sondh, mkurugenzi katika hoteli hiyo, ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa hakukutokea uharibifu wowote akisema mlipuko ulitokea upande wa baharini katika eneo lililotengwa kwa ajili ya umma karibu na ilipo hoteli hiyo. Wizara ya mambo ya ndani ya Kenya awali ilisema mlipuko huo ulikuwa umetokea katika lango la hoteli ya Reef, lakini msemaji wa wizara hiyo, Mwenda Njoki, akafafanua baadaye kuwa mlipuko huo ulikuwa umetokea upande wa ufukoni.

Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na mashambulizi hayo lakini maafisa wa Kenya wamelinyoshea kidole cha lawama kundi la al Shabaab kutoka Somalia kwa mashambulizi kadhaa, likiwemo shambulizi dhidi ya jengo la maduka la Westgate Septemba mwaka uliopita ambapo watu 67 waliuwawa. Kutoka wakati huo kumetokea msururu wa mashambulizi.

Kenya iliwatuma wanajeshi wake Somalia mwaka 2011 kujaribu kuwakabili wapiganaji wa al Shabaab ambao inawaona kama kitisho kwa mipaka yake na usalama wa taifa. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amesema sekta ya utalii ilikuwa imekwama kutokana na mashambulizi ya wanamgambo wanaotaka wanajeshi wa nchi hiyo waondoke Somalia. Kenyatta amekataa sharti lao. Mji wa Mombasa ni kivutio muhimu cha watalii na pia kuna bandari kubwa kwa ajili ya eneo zima la Afrika Mashariki, iliyopo katika pwani ya bahari ya Hindi.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com