1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto nchini Uganda wasifia maisha ya wakati wa vita

Isaac Gamba
13 Aprili 2017

 Watoto ambao mama zao walibakwa na waasi wa Lords Resistance Army (LRA) nchini Uganda wanasema kipindi cha  vita kilikuwa ni bora zaidi kwao kuliko  hivi sasa.

https://p.dw.com/p/2bBO4
Uganda - ein Junge zeigt Verletzungen durch die LRA
Picha: AP

Watafiti kutoka chuo kikuu cha MCGill nchini Canada waliwahoji watoto 60 waliochukuliwa mateka na waasi wa Lords Resistance Army (LRA) ambao walifanya vitendo vibaya vya ukatili  nchini Uganda katika kipindi cha miongo miwili hadi mwaka 2005 waasi hao walipofurushwa kutoka nchini humo.

"Ukweli unaoelezewa na watoto hao wakiainisha hali ya wakati wa vita wakati walipokuwa wakikabiliwa na hali mbaya ya vurugu, mateso pamoja na njaa kuwa ni bora zaidi maisha ya wakati huo kuliko maisha yao ya sasa " Anasema Myriam Denov  kutoka chuo kikuuu cha McGill  ambaye ni kiongozi wa utafiti huo katika taarifa yake aliyoitoa Jumanne wiki hii.

Watoto hao ambao baadhi yao baba yao ni  kiongozi wa waasi Joseph Kony walionekana kuwa na nyuso zilizo jaa huzuni baada ya vita.

Mmoja wa watoto hao alisikika akisema familia yao inawachukia yeye na wenzake wawili  waliozaliwa wakati wa kipindi ambacho mama yao alikuwa mateka na kuwa mjomba wao huwapiga sana na kusisitiza kuwa atawaua.

Watoto hao wanasema familia yao na jamii kwa ujumla wanawaona kuwa watu hatari, wakiwachukulia kuwa ni watoto waasi ambao wameleta mkosi katika jamii na pepo wabaya kutoka msituni.

 

           Waasi wa Lord's Resistance army wanadaiwa kuwakata viungo raia

Lord Resistance Army in Uganda
Baadhi ya wapiganaji wa kundi la Lord's Resistance Army nchini UgandaPicha: AP Photo

Kundi la waasi la LRA nI kundi ambalo hufanya  vitendo vya kikatili ikiwa ni pamoja na kuwakata viungo raia pamoja na kuwateka nyara watoto huku likiwatumia kama wapiganaji na watoto wengi walilazimishwa kuwaua ndugu zao ndani ya familia pamoja na marafiki.

Dominic Ongwen ambaye ni kamanda wazamani wa kundi hilo la Lords Resistance Army aliyekamatwa wakati akiwa bado na umri mdogo na kulazimishwa kujiunga na waasi hao  hivi sasa anakabiliwa na mashitaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu.

 Utafiti huo umebainisha kuwa watoto waliozaliwa baada ya mama zao kubakwa katika kipindi hicho walikuwa chini ya uangalizi mzuri wa baba zao ambao ni waasi waliohakikisha kuwa  wanapata mahitaji muhimu ambayo hawayapati  wakati wa kipindi cha amani.

Mmoja wa watoto anasema kuwa maisha hayakuwa mabaya zaidi kipindi hicho kwa sababu mzazi wake wa kiume alihakikisha kuwa anapata chakula na anasema alipendwa sana na baba yake huyo muasi.

Waasi wa LRA wanaendesha harakati zao katika mipaka ya Sudani, Jamhuri ya KIdemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu walipofurushwa nchini humo na jeshi la Uganda.

Mwandishi: Isaac Gamba/ RTRE

Mhariri      :Yusuf Saumu