1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto kiasi 300 waliotekwa nyara Nigeria waachiliwa

Saumu Mwasimba
24 Machi 2024

Eneo la Kaskazini mwa Nigeria limekithiri matukio ya utekaji nyara watoto wa shule unaofanywa na makundi ya itikadi kali na magenge ya kihalifu

https://p.dw.com/p/4e4Vj
Nigeria Schulkinder Entführung Eltern
Picha: Sunday Alamba/AP Photo/picture alliance

Kundi la watoto takriban 300 waliotekwa nyara kutoka shuleni walikokuwa wakisoma na watu wenye silaha wameachiwa huru. Watoto hao walitekwa nyara wiki mbili zilizopita Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.

Kuachiliwa huru kwa watoto hao kumetangazwa leo Jumapili na serikali ya jimbo la Kaduna kupitia ujumbe uliochapishwa kwenye ukrasa wa X ambapo gavana wa jimbo hilo Uba Sani amesema watoto hao wako salama baada ya kuachiliwa kufuatia operesheni za mashirika ya kiusalama ambayo yamefanikisha hatua hiyo. 

Kumbukumbu ya tukio

Shule ya  Kuriga Nigeria
Darasa la shule ya Kuringa ambako watoto 250 walitekwa nyaraPicha: Haidar Umar/AFP

Kundi lenye silaha liliishambulia shule ya msingi na sekondari katika kijiji cha Kuringa March 7 na kuwateka nyara wanafunzi 287 wavulana na wasichana.

Kwa mujibu wa mwalimu aliyezungumza na kituo kimoja cha televisheni katika eneo hilo,jengo la shule lilizingirwa na watu waliojihami kwa silaha muda mfupi kabla ya shughuli za masomo kuanza mapema asubuhi.

Watu hao waliwalazimisha wanafunzi takriban 700 na walimu kuelekea kwenye eneo la kichaka. Hata hivyo wengi wa wanafunzi pamoja na walimu walifanikiwa kutoroka.

Maeneo ya kati na Kaskazini mwa Nigeria, nchi ambayo ina idadi ya wakaazi wengi zaidi barani Afrika,yamekuwa yakishuhudia matukio ya utekaji nyara mara kwa mara, yanayofanywa na magenge ya wahalifu na hata makundi ya itikadi kali ya kigaidi.Soma pia:Watu wengine karibu 100 watekwa nyara na wahalifu nchini Nigeria

Matukio ya nyuma ya utekaji nyara

Miaka takriban 10 iliyopita mnamo mwaka 2014 tukio jingine la utekaji nyara lililosababisha kilio kimataifa lilitokea nchini Nigeria. Wasichana 276 wa shule walitekwa nyara na kundi la Boko Haram katika eneo la Chibok Kaskazini- Mashariki mwa nchi hiyo kwenye mkoa wa Borno. Bado wasichana chungunzima hawajapatikana.

Shule ya Kuringa ikilindwa Kaduna Nigeria
Jeshi likitowa ulinzi kwenye shule-Kaduna NigeriaPicha: Sunday Alamba/AP/picture alliance

Kundi la itikadi kali la Boko Haram na makundi mengine ya jihadi mara nyingi huwateka nyara watoto wakike na wanawake kutowa madai yao ya kisiasa, na huwatumia wasichana hao kwa kuwaingiza kwenye ndowa za lazima au kuwatumia kingono na kuwafanya watumwa wa kazi za ndani.

Kwa upande mwingine magenge huwatumia wasichana hao kuitisha fedha za kigombozi . Kwa mujibu wa taasisi inayohusika na masuala ya kutowa ushauri kuhusu  uchumi na usalama  ya SB Morgen,kulipwa kigombozi,ndio sababu kubwa ya utekaji nyara kutokana na mgogoro wa kiuchumi unaoshuhudiwa Nigeria.

Taasisi hiyo inasema watu 3,620  walitekwa nyara katika matukio 582  nchini Nigeria katika kipindi cha miezi 12,kuanzia Julai 2022 hadi Juni 2023 peke yake.Na makutukio mengi yaliripotiwa katika jimbo la Kaduna.

Na kimsingi eneo ambako kuna shule hutazamwa kama eneo lenye hatari ya kukabiliwa na uhalifu.Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni makundi madogo ya watu na zaidi ya wanawake na watoto yamekuwa yakilengwa mara kwa mara ya utekaji nyara katika mkoa huo.