Watoto 300 wanakufa kila siku katika nchi za mizozo | Masuala ya Jamii | DW | 15.02.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Watoto 300 wanakufa kila siku katika nchi za mizozo

Njaa, magonjwa na ukosefu wa misaada vinawaua takriban watoto 300 kila siku katika mataifa yanayokumbwa na mizozo duniani, huku idadi ya watoto wanaojikuta katikati ya mizozo ikizidi kuongezeka.

Shirika la kimataifa la kuwahudumia watoto la Save the Children limesema watoto wasiopungua laki moja wanakufa kila mwaka kutokana na vita na athari zake kuanzia kukumbwa na njaa, kuuawa hadi kunyimwa misaada.

Inakadiriwa watoto wachanga laki tano walifariki dunia kutokana na mapigano kati ya mwaka 2013 hadi 2017. Nchi ambazo watoto wanaathirika zaidi ni Afghanistan, Yemen, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya kati na Syria. Nchi nyingine ni Nigeria, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Iraq, Mali.

Kulingana na data kutoka Umoja wa Mataifa zilizokusanywa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kwa jumla watoto laki tano walikufa kutokana na njaa, hospitali na miundo mbinu muhimu kushambuliwa, na kupunguzwa kwa misaada ya kibinadamu, takwimu hizo zikiwa hazigusii watoto waliouawa katika mashambulizi.

Vita vinawaathiri zaidi watoto

Kulingana na ripoti iliyotolewa na jarida la kitabibu la Lancet mwaka jana, Watoto milioni tano barani Afrika wamefariki dunia katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita katika mataifa ya mizozo kwa kukosa huduma za afya au maji safi.

Afrika Flucht Daryeel Kamp in Mogadishu (picture-alliance/AP Photo/Abdi Warsameh)

Watoto wa Kisomali waliokimbilia usalama katika kambi ya Dadaab-Kenya

Afisa Mkuu wa Save the Children Kevin Watkins anasema kuanzia Yemen, Syria hadi Sudan Kusini, watoto wanakabiliwa na makali ya vita.

Akizindua ripoti hiyo katika kongamano la usalama la Munich leo, mkurugenzi mkuu mtendaji wa shirika hilo la kutoa misaada kwa watoto Helle Thornig Schmidt amesema kati ya watoto watano duniani, mmoja anaishi katika nchi iliyo na mzozo na kuongeza wanatiwa wasiwasi na kuongezeka kwa visa vya kuzuiwa kwa misaada kama silaha vitano.

Ulimwengu wahimizwa kuchukua hatua zaidi

Schmidt amesema inashtusha kuwa katika karne hii ya 21 ulimwengu unarudi nyuma kuhusu misingi na maadili ya kimsingi kama watoto na raia hawapaswi kamwe kulengwa katika vita na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti kuwalinda watoto duniani.

Inakadiriwa kufikia mwaka 2017, watoto milioni 420 walikuwa wanaishi katika nchi zinazokumbwa na mizozo, hiyo ikiwa ongezeko la watoto milioni 30 ikilinganishwa na mwaka 2016 na ikiorodheswa idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika mazingira ya mizozo kuwahi kuripotiwa tangu mwaka 1990.

Maovu mengine yanayowakumba watoto ni kulazimishwa kujiunga katika vita kama wapiganaji, kunyanyaswa kingono, kutumika kama washambuliaji wa kujitoa muhanga, kutekwa nyara, kulemazwa na kunyimwa chakula.

Save the Children imesema vita dhidi ya watoto ni sharti vikomeshwe na wanaohusika na maovu hayo kuchukuliwa hatua.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Thomson Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com