1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina 153 waruhusiwa kutoka kwenye ndege Afrika Kusini

14 Novemba 2025

Zaidi ya Wapalestina 150, waliozuiwa ndani ya ndege kwa saa 12 na polisi wa mpaka wa Afrika Kusini, waliruhusiwa jana jioni kutoka kwenye ndege hiyo. Haya ni kulingana na mamlaka ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/53bYm
Uwanja wa ndege wa Afika Kusini
Ofisi za tiketi za ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa O.R. Tambo nchini Afrika KusiniPicha: MICHELE SPATARI/AFP/Getty Images

Polisi inasema ndege hiyo iliyokuwa imewabeba Wapalestina 153 ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa O.R Tambo muda mfupi baada ya saa mbili asubuhi kwa saa za eneo hilo.

Pia imesema, abiria hao hawakuruhusiwa kuondoka kwenye ndege kwa vile hawakuwa na mihuri ya kawaida inayoonyesha wametoka eneo fulani na kuongeza kuwa hakuna aliyeelezea nia ya kuomba hifadhi.

Wapalestina 23 walikuwa wanasubiri kuelekea kwingineko

Jumla ya abiria 130 waliingia nchini humo na 23 walikuwa wakingoja kuunganisha safari zao kulekea eneo lingine.

Hatimaye Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hiyo iliidhinisha kushuka kwa abiria hao baada ya Shirika lisilo la kiserikali la Gift of the Givers kuhakikisha kuwa litawapa abiria makaazi ya muda.

Haikubainika wazi Wapalestina hao wamesafiri chini ya mazingira gani na walikokuwa wakielekea.