1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasiasa wa Israel washutumiwa kuuchochea mzozo Jerusalem

Admin.WagnerD6 Novemba 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Israel amewashutumu wanasiasa wa mrengo wa kulia kwa kuuchochea mzozo unaondelea mjini Jerusalem ambako hofu imetanda kuwa ghasia zinazozidi kuhusu eneo takatifu huenda zikashindwa kudhibitiwa

https://p.dw.com/p/1DiFj
Picha: Ahmad Gharabli/AFP/Getty Images

Matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman yanakuja siku moja tu baada ya mwanamgambo wa kundi la Hamas kuugonga kwa gari umati wa watu waliokuwa wakisubiri kuabiri treni mjini Jerusalem na kumuua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine 13 huku raia mmoja wa Palestina naye akiwagonga wanajeshi wa Israel katika ukingo wa magharibi na kuwajeruhi vibaya wanajeshi watatu.

Polisi ya Israel imesema imeanza kuweka vizuizi katika barabara ya kuelekea vituo vya treni mjini Jerusalem ili kuzuia visa kama hivyo vya washambuliaji kutumia magari yao kuwagonga abiria.

Msikiti wa Al Aqsa wazozaniwa

Mzozo wa mara kwa mara katika eneo takatifu mjini Jerusalem ambako kuna msikiti wa Al Aqsa unaong'anganiwa na wayahudi na waislamu kila upande ukidai kuwa na haki ya kuabudu ndani ya msikiti huo umeongezeka katika wiki za hivi karibuni huku wanasiasa wenye misimamo mikali wa Israel wakitaka kuondelewa kwa vikwazo vinavyowazuia wayahudi kutosali katika msikiti huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman
Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor LiebermanPicha: Reuters

Lieberman hii leo amesema wanasiasa wa nchi yake wanaotaka wayahudi wapewe haki zaidi za kuomba katika eneo hilo takatifu wanajiendesha katika hali ambayo si ya kuwajibika na nia yao ni kujipatia tu umaarufu wakati mazingira yakiwa tete.

Lieberman mwenyewe ni mwanasiasa asiye na msimamo wa kidini lakini mwenye siasa kali na katika kipindi cha nyuma ametoa matamshi ambayo ni hasi kuhusu wapalestina na waisrael waarabu lakini katika miezi ya hivi karibuni ameonekana kuwa na msimamo wa wastani.

Palestina yataka Israel kuwajibishwa

Mwakilishi wa Palestina katika umoja wa Mataifa Riyad Mansour amesema baraza la usalama lazima litangaze msimamo wake kuitaka serikali ya Israel kusitisha vitendo na sera ambazo ni za kichokozi na zinazochochea uhasama.

Mwakilishi wa Palestina katika umoja wa Mataifa Riyad Mansour
Mwakilishi wa Palestina katika umoja wa Mataifa Riyad MansourPicha: picture alliance/AP Photo

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amelaani shambulizi hilo lililotokea jana na kulitaja kitendo cha ugaidi ambacho kinazidi kuchochea uhasama katika kanda inayokumbwa na msukosuko.

Mkuu wa masuala ya kigeni wa umoja wa Ulaya Federica Mogherini amezitaka pande zote katika mzozo huo wa mashariki ya kati kuonyesha uvumilivu na kulitaja shambulizi hilo kuwa thibitisho wazi la kuwepo haja ya kuchukuliwa hatua zaidi zitakazohakikisha makubaliano ya amani ya kudumu yanafikiwa kuhusu mzozo kati ya Israel na Palestina.

Makabiliano zaidi yanatarajiwa leo wakati kundi la waisraeli wa mrengo wa kulia wenye itikadi kali wakipanga kuandamana hadi malango ya msikiti wa Al Aqsa karibu na alipopigwa risasi kiongozi wa kidini mwenye msimamo mkali wa kiyahudi Yehuda Glick wiki iliyopita.

Mwandishi:Caro Robi/ap/afp

Mhariri: Yusuf Saumu