Wanaoikimbia Syria sasa wafikia 10,000 | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wanaoikimbia Syria sasa wafikia 10,000

Syria inaendelea kushinikizwa isitishe misako inayofanywa na vikosi vya serikali dhidi ya waandamanaji wanaotaka demokrasia, huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa kiasi ya raia 10,000 wameshaikimbia nchi hiyo.

Wakimbizi wa Syria nchini Uturuki

Wakimbizi wa Syria nchini Uturuki

Hivi leo (14.06.2011), vikosi vya Syria vinaendelea na operesheni yao kali ya nchi kavu katika milima ya kaskazini mwa nchi hiyo, lakini wakimbizi waliokimbia na kuingia Uturuki wamesema baadhi ya wanajeshi wanaiasi operesheni hiyo katika juhudi za kuwalinda raia.

Televisheni ya taifa imesema maafisa wawili wakuu wa kijeshi wanachunguzwa kuhusiana na jukumu walilotekeleza katika msako wa awali, huku viongozi wa kimataifa wakiendelea kuishtumu operesheni hiyo ya serikali dhidi ya waandamanaji.

Baadhi ya maelfu ya wakimbizi waliokimbia hadi nchi jirani ya Uturuki walisema wanajeshi waliyachoma moto mashamba na kuwachinja mifugo katika vijiji vilivyo karibu na mpaka.

Televisheni ya taifa ilisema jeshi lilikuwa likiyasaka magenge ya watu waliojihami ndani ya misitu na milima iliyoko karibu na Jisr al Shungur baada ya kuuvamia mji huo, ambao umekuwa kitovu cha maandamano mwishoni mwa wiki.

Mtoto wa Kisyria akionesha risasi kutoka bunduki za wanajeshi

Mtoto wa Kisyria akionesha risasi kutoka bunduki za wanajeshi

Watetezi wa haki za binaadamu waliripoti milio mikubwa ya risasi na miripuko mjini humo jumapili usiku, wakati wanajeshi waliosaidiwa na helikopta za mizinga na karibu vifaru 200 wakizindua mashambulizi mawili makubwa hadi asubuhi.

Hapo jana waliripoti kuwepo kwa milio ya risasi wakati vikosi vilipoanzisha operesheni katika kijiji cha Uram al Joz, mashariki ya Jisr al Shungur, na milima ya Jebel al Zawiya ya upande wa kusini.

Lakini wengi wa wakaazi 50,000 wa mji huo walikuwa tayari wameondoka wakati wa kipindi cha wiki nzima cha matayarisho ya msako huo.

Baadhi ya wale waliokimbia hadi Uturuki walieleza jinsi jeshi la syria lilivyofanya operesheni kali ya nchi kavu mjini Jisr al Shungur na vijiji vingine vya mkoa wa Idlib.

Watoto wa Kisyria wakiwa ukimbizini nchini Uturuki

Watoto wa Kisyria wakiwa ukimbizini nchini Uturuki

Zaidi ya Wasyria 6,800 wametafuta hifadhi nchini uturuki, kiasi cha kilomita 40 kutoka mji wa Jisr al Shungur. Wengine 5,000 wameingia nchini Lebanon, haya ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema raia wa Syria wanapaswa kuhakikishiwa usalama wao watakaporejea makwao.

Wakati huo huo, mjini Washington maafisa wamemtaka rais Bashar al Assad aunde serikali ya mpito au ajiuzulu, huku mataifa ya magharibi yakighadhabishwa na kutokuwepo kwa umoja katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ili kuishtumu Syria.

Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Gerard Araud, alilalamika kuwa wiki mbili za mgogoro wa kidiplomasia kuhusu azimio la kuushtumu msako wa Syria zimegharimu kupotea kwa maisha ya watu wengi.

Marekani inaunga mkono azimio hilo la Ulaya, lakini wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa walio na nguvu, Urusi na China, wamelipinga. Hata walisusia mazungumzo ya hapo jana kuhusiana na azimio hilo.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jay Carney, ameshtumu msako huo, akisema serikali ya mpito inapaswa kuundwa na ikiwa Rais Assad hataongoza kuundwa kwa serikali hiyo, basi inabidi ajiuzulu.

Mwandishi: Bruce Amani/ AFP
Mhariri: Miraji Othman

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com