1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duru ya pili ya uchaguzi kuamua rais mpya Sao Tome

Saumu Mwasimba
5 Septemba 2021

Sao Tome na Principe ni nchi ya visiwa inayotazamwa kama mfano wa nchi inayofuata demokrasia inayozingatia sheria katika eneo la Afrika ya Kati

https://p.dw.com/p/3zw3h
Portugal Wählerregistrierung für Wahlen in Sao Tome und Principe
Picha: Botschaft von Sao Tome und Principe in Lissabon/DW

Wananchi wa nchi ya visiwa vya Sao Tome na Principe wanapiga kura leo Jumapili katika uchaguzi wa duru ya pili, ukiwa ni mchuano kati ya aliyekuwa waziri wa miundo mbinu Carlos Vila Nova, aliyeshinda katika duru ya mwanzo iliyofanyika mwezi Julai na waziri mkuu wa zamani Guilherme Posser da Costa.

São Tomé und Príncipe Präsidentschaftswahlkampf 2021 | Carlos Vila Nova
Picha: Ramusel Graça/DW

Sao Tome ambayo inaangaliwa kama mfano wa nchi inayofuata mfumo wa demokrasia unaozingatia sheria katika pwani ya eneo la Afrika ya Kati pia  ni nchi yenye maslahi kwa sekta ya mafuta yakishuhudiwa makampuni chungunzima ya uchimbaji mafuta yaliyoweka matumaini ya kupata hifadhi ya mafuta nchini humo.

Wananchi 123,000 wenye vigezo vya kupiga kura,waliojiandikisha watamchagua rais mpya atakayemrithi Evaristo Carvalho mwenye umri wa miaka 79 ambako hakugombea muhula mwingine wa miaka mitano katika nafasi hiyo ambayo kimsingi haina mamlaka makubwa.

Duru hii ya pili ya uchaguzi wa rais ilicheleweshwa wakati mgombea wa nafasi ya tatu Delfim Neves alipodai umefanyika udanganyifu na kutaka kura zihesabiwe upya.Duru hii ya pili mwanzoni ilipangwa kufanyika Agosti 8 ukaaghirishwa hadi Agosti 29 na kisha kucheleweshwa tena baada ya malalamiko ya udanganyifu yaliyotolewa na Delfim Neves.

São Tomé und Príncipe Präsidentschaftswahlkampf 2021 | Dellfim Neves
Picha: Ramusel Graça/DW

Lakini mwishowe mahakama ya katiba nchini humo ilikataa ombi lake. Kuna vituo 262 vya kupiga kura katika nchi hiyo nzima ambayo ni koloni la zamani la Ureno katika ghuba ya Guinea na vituo hivyo vitafungwa saa moja usiku kwa saa za Ulaya ya Kati.

Ikumbukwe kwamba katika kipindi cha miongo miwili iliyopita kwa mujibu wa benki ya dunia,ukuaji katika nchi hiyo umechochewa zaidi na bajeti ya matumizi ya serikali ikisaidiwa na msaada kutoka nje  na mikopo iliyochukuliwa na serikali pamoja na kilimo,utalii na uwekezaji wa kigeni katika sekta ya uchimbaji mafuta.

Sao Tome na Principe iliingia kwenye mfumo wa vyama vingi 1991 baada ya miaka 15 ya utawala wa chama kimoja wa serikali ya Kimaxist . Carlos Vila Nova ni kiongozi wa chama cha upinzani cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha Independent Democratic Action ADI na aliongoza katika matokeo ya duru ya kwanza Julai 18 kwa kupata asilimia 39.5 ya kura. Ni mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 62 na alikuwa waziri wa miundo mbinu lakini ni miongoni mwa watu ambao hawajulikani sana na umma. 

São Tomé und Príncipe Präsidentschaftswahlkampf 2021 | Pósser da Costa
Picha: Ramusel Graça/DW

Mpinzani wake wa karibu Gulherme Posser da Costa mwenye umri wa miaka 68 anatokea chama cha siasa za wastani za mrengo wa shoto,kinachojulikana kama chama cha ukombozi wa Sao Tome na Principe MLSTP,alipata asilimia 20.7 katika duru ya kwanza. Chama chake ndicho kinachoongoza muungano tawala  katika bunge la nchi hiyo.

Rais hana madaraka makubwa nchini humo bali jukumu lake ni la usuluhishi katika mivutano ya kisiasa,madaraka makubwa yako kwa waziri mkuu ambaye hivi sasa ni Jorge Lopes Bom Jesus kutoka chama cha MLSTP kilichoshinda uchaguzi wa 2018.