Wamarekani wamotishwa kukabiliana na wakati mgumu | Magazetini | DW | 26.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Wamarekani wamotishwa kukabiliana na wakati mgumu

Mada iliyogonga vichwa vya habari katika magazeti mengi ya Ujerumani leo Alkhamisi ni hotuba iliyotolewa na Rais wa Marekani Barack Obama Jumanne usiku ambayo haikuwahi kuchambuliwa na magazeti hiyo jana.

Mishahara minono na marupurupu ya mameneja ni mada nyingine inayochomoza takriban kila siku magazetini. Lakini tutaanzia na hotuba ya Obama iliyovutia wengi si nchini Marekani tu. Gazeti la TRIERISCHE VOLKSFREUND linaandika:

"Barack Obama Jumanne usiku alijitokeza mbele ya bunge la Marekani kama msaikolojia mkuu wa taifa zima.Ujumbe wake mkuu ni huu: Si kawaida kwa Mmarekani kukata tamaa,atakabiliana na wakati huu mgumu na atafanikiwa hata taifa litaibuka imara kutoka janga la kiuchumi. Kile anachojaribu kufanya Obama ni kuwatia moyo wananchi wanaokabiliwa na wakati mgumu."

Na gazeti la OSTSEE ZEITUNG likiendelea na mada hiyo linasema:

"Kiongozi anaetegemewa sana na wananchi ameahidi kuwa Marekani itaibuka imara kuliko hapo zamani. Matumaini kama hayo wakati huu wa dhiki,ni kitu kigeni kwa Wajerumani wenye tabia ya kutafakari. Lakini historia ya Marekani,mara nyingi imedhihirisha kuwa nchi hiyo ina uwezo wa ajabu."

Lakini kuna suali moja.Je,hao waliosababisha msukosuko wa fedha na uchumi wapo tayari kushirikiana na taifa kujitoa katika janga hilo? Kwani sasa ndio inaanza kazi kubwa ya kugawana mzigo huo.

Tukiendelea na uhariri wa magazeti ya Ujerumani ndio tunaangukia kwenye mada ya marupurupu yanayolipwa kwa mameneja wa benki na makampuni makubwa.Gazeti la EXPRESS kutoka Cologne limeandika hivi:

Mara nyingi mameneja hata bila ya kufanya kazi kwa ufanisi, hulipwa mishahara minono.Utafiti uliofanywa na serikali umefichua jinsi pesa zinavyochezewa ovyo katika makampuni mengi.Ni sahihi kuwa mamaneja wanaofanya kazi zao vizuri,wanastahili pia kulipwa mishahara minono.

Lakini ni haki kweli kwa mishahara hiyo kuwa mara 300 au hata mara 1000 zaidi ya mshahara wa wastani anaelipwa mfanyakazi wa kawaida? Hapo hakuna uwiano wo wote lasema gazeti la EXPRESS.

Si hilo tu - kero zaidi ni kuona vipi wakuu hao husababisha hasara kubwa bila ya kuwa na hofu ya kuadhibiwa.Kwani mara nyingi badala ya kuadhibiwa,mameneja hao huondoka baada ya kupokea kitita cha fedha. Wahanga ni wafanyakazi wanaopoteza ajira na wale wanaomiliki hisa katika makampuni yaliyotumbukizwa matatani kwa sababu ya uongozi mbaya.Hao ndio watakaobeba mzigo mzima wa hasara iliyosababishwa na mameneja waliyojipatia marupurupu kabla ya kutoweka.

 • Tarehe 26.02.2009
 • Mwandishi P.Martin. - (DPA)
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H1eV
 • Tarehe 26.02.2009
 • Mwandishi P.Martin. - (DPA)
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H1eV