1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walioambukizwa virusi vya Corona China wapindukia 70,000

Sylvia Mwehozi
17 Februari 2020

Idadi ya walioambukizwa virusi vipya vya Corona nchini China imepindukia 70,000 mnamo wakati wataalamu wa kimataifa wakianza kukutana na wenzao wa China juu ya mripuko wa virusi hivyo .

https://p.dw.com/p/3XsLW
China | Coronavirus
Picha: picture-alliance/dpa/XinHua/Z. Yuwei

Idadi ya visa vipya vya mripuko wa ugonjwa huo imepungua kwa siku ya tatu mfululizo ingawa ulimwengu umesalia katika tahadhari kubwa juu ya kusambaa kwake kulikotiliwa mkazo na tangazo la Marekani kwamba raia wake zaidi ya 30 waliokuwamo ndani ya meli iliyowekwa karantini nchini Japan wana maambukizi ya virusi hivyo.

Idadi ya vifo imeongezeka na kufikia 1700 China bara baada ya watu wengine 142 kupoteza maisha. Zaidi ya watu 70,000 sasa wameambukizwa virusi hivyo ingawa kwa ujumla kesi mpya za virusi vya coronavilivyopewa jina la COVID-19 imeendelea kupungua. Jimbo la Hubei ambako ndiko vilikoanzia virusi hivyo limeanzisha hatua mpya na kali zinazokusudia kudhibiti maambukizi zaidi.

Hatua hizo ni pamoja na kuwafungia wakaazi na kuhakikisha wanadhibiti watu kutembea kwa saa 24, kuzuia magari yote barabarani isipokuwa tu yale ya huduma za dharura, magari maalum yanayosafirisha bidhaa muhimu pamoja na kulazimisha usajili wa majina wakati wa kununua dawa baridi kutoka maduka ya madawa.

Japan | Coronavirus | Kreuzfahrtschiff «Diamond Princess»
Meli ya Diamond Princess iliyowekwa karantini mjini YokohamaPicha: picture-alliance/dpa/kyodo

Nao wataalamu wa kimataifa wanaoshiriki katika ujumbe unaongozwa na shirika la afya duniani WHO wamewasili mjini Beijing na tayari wamekutana na wenzao wa China, amesema mkuu wa shirika la afya ulimwenguni Tedros Adhanom Ghebreyesus ingawa ameonya kwamba "ni vigumu kutabiri mwelekeo wa mripuko huo".

Wakati huo huo Marekani imewaondoa raia wake kutoka kwenye meli iliyowekwa karantini nchini Japan siku ya Jumatatu , wakati mataifa mengine nayo yakijiandaa kuchukua hatua kama hizo. Nje ya China maambukizi makubwa yanapatikana kwenye meli ya Diamond Princess ambako visa vya maambukizi vimepanda hadi 355 licha ya abiria kufungiwa kwenye vyumba vyao wakati wa siku 14 za kuwekwa chini ya karantini.

Australia ni nchi nyingine iliyotangaza kuwaondoa raia wake zaidi ya 200 walioko kwenye meli hiyo. Waziri mkuu Scott Morrison amesema abiria hao wataondolewa Jumatano ya wiki hii na kupelekwa eneo la tropiki kaskazini mwa nchi hiyo, ambako watakaa huko kwa siku 14 kwa uangalizi zaidi. Meli hiyo ya Diamond Princess imekuwa chini ya karantini tangu kuwasili kwake mjini Yokohama Februari 3.

Vyanzo: AFP/DPA/Reuters