Kaunti zaidi ya 10 nchini Kenya zakumbwa na uhaba wa chakula
28 Januari 2026
Zaidi ya watu milioni mbili nchini Kenya wanakabiliwa na hatari ya uhaba wa chakula kufuatia mvua chache za msimu wa vuli ambazo hazijashuhudiwa kwa zaidi ya miongo minne. Hali hii imeathiri pakubwa maeneo ya wafugaji na kaunti zilizoko katika ukanda wa ukame.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maeneo ya Ukame (NDMA), zaidi ya kaunti kumi zinapambana na uhaba wa maji na maeneo ya malisho, hali inayozidi kudhoofisha maisha ya jamii zinazoitegemea mifugo.
Mvua za vuli za mwaka 2025 zilinyesha kwa kiwango cha asilimia 30 hadi 60 pekee ya kiwango kilichotarajiwa, hasa katika maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Kenya.
Mifugo, ambayo ni rasilimali kuu kwa jamii za wafugaji, imeathirika pakubwa kutokana na uhaba wa maji na malisho, jambo linaloongeza hatari ya njaa na utapiamlo.
Hali hiyo imewaweka katika mazingira magumu zaidi watoto na kina mama wajawazito katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Kongamano la wafugaji laweka jamii katikati ya suluhu
Wakati huohuo, kongamano la kwanza la wafugaji na walezi wa maeneo ya mbuga limekamilika nchini Kenya, likiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Wafugaji na Usimamizi wa Maeneo ya Mbuga (IYRP), uliotengwa na Umoja wa Mataifa.
Kongamano hilo la siku tano limewaleta pamoja wadau kutoka jamii za wafugaji, wataalamu wa mazingira na viongozi wa serikali ili kujadili changamoto na suluhu endelevu kwa maisha ya wafugaji.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Waziri wa Ulinzi wa Kenya, Soipan Tuya, alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuandaa sera na sheria jumuishi zinazowapa wafugaji nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayowahusu.
Alibainisha kuwa hatua hizo zimeimarisha mchango wa jamii za wafugaji katika sera za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza maeneo ya mbuga.
Kwa mujibu wa serikali, kuwashirikisha wafugaji kunalenga kuhakikisha haki zao zinalindwa huku wakichangia uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya kitaifa.
Athari za ukame zatanda ukanda wa Afrika Mashariki
Athari za ukame zimeanza pia kushuhudiwa katika nchi jirani za Somalia, Tanzania na Uganda, hali inayozua wasiwasi wa mgogoro wa chakula katika eneo zima la Afrika Mashariki.
NDMA inasema kaunti 13 zilizo kwenye maeneo ya kupokea mvua kidogo tayari zimeonyesha dalili za kuathiriwa na ukame, hasa katika upatikanaji wa maji na afya ya mifugo.
Serikali ya Kenya imeonya kuwa hadi watu milioni 2.5 wako katika hatari ya kukumbwa na njaa kali endapo kiangazi kitaendelea kwa muda mrefu.
Kwa jamii nyingi za wafugaji, shughuli za kila siku zimekuwa ngumu zaidi kutokana na umbali mrefu wa kutafuta maji na malisho.
Baadhi ya wafugaji wameanza kutumia mbinu mbadala kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kupanda nyasi na kuzihifadhi kwa matumizi ya wakati wa kiangazi.
Grace Meitiaki, mkazi wa Laikipia, ni miongoni mwa wafugaji waliobuni njia ya kutengeneza malisho yaliyohifadhiwa kwa mfumo wa madonge yenye virutubishi muhimu kwa mifugo.
Anasema mafunzo aliyopata yalimsaidia kuelewa kuwa nyasi zinaweza kupandwa, kuvunwa na kuhifadhiwa ili kusaidia mifugo wakati wa vipindi vya ukame.
Kwa kutumia mbinu hiyo, wafugaji wameanza kupunguza vifo vya mifugo na kulinda chanzo chao kikuu cha kipato.
Wafugaji wasubiri mvua za masika
Hata hivyo, jamii nyingi za wafugajibado zinaelekeza matumaini yao kwa mvua za masika zinazotarajiwa kunyesha kati ya Machi na Mei.
Wataalamu wa hali ya hewa wanasema mvua hizo zitakuwa muhimu katika kurejesha vyanzo vya maji na kuboresha hali ya malisho katika maeneo yaliyoathirika.
Kongamano la wafugaji na walezi wa maeneo ya mbuga linatarajiwa kuhitimishwa kwa kikao cha kilele kitakachofanyika Mongolia baadaye mwaka huu.
Kikao hicho kitaadhimisha rasmi Mwaka wa Kimataifa wa Wafugaji na Usimamizi wa Maeneo ya Mbuga (IYRP), huku kikilenga kutambua mchango wa jamii hizo katika usalama wa chakula na uhifadhi wa mazingira duniani.