Wakazi wa vijiji vya Marsabit wataka ulinzi uimarishwe | Matukio ya Afrika | DW | 27.12.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wakazi wa vijiji vya Marsabit wataka ulinzi uimarishwe

Wakaazi kwenye vijiji vinavyokaribiana na mpaka wa Kenya na Ethiopia jimboni Marsabit, Kenya wanatoa wito kwa serikali ya nchi yao kuimarisha ulinzi wa eneo hilo.

Wakaazi wanaoishi kwenye vijiji vinavyokaribiana na mpaka wa Kenya na Ethiopia jimboni Marsabit nchini Kenya wanatoa wito kwa serikali ya nchi yao kuimarisha ulinzi wa eneo hilo, kufuatia kisa cha hivi karibuni kabisa ambapo majeshi ya polisi kutoka Ethiopia yaliingia vijijni mwao na kufanya mashambulizi yaliyopelekea familia zaidi ya mia tano kukimbia wakihofia usalama wao. 

DW ilipofika kwenye eneo hili la mpaka kati ya Kenya na Ethiopia, iliambiwa na wanakijiji kwamba wanajeshi kutoka Ethiopia walivuuka mpaka mwishoni mwa wiki iliyopita na kuingia katika vijiji vya Wayye Goda, Anona na Mado Ado katika jimbo la Moyale, kwa madai ya kuwasaka wapiganaji wa kundi la waasi la OLF na kisha kuteketeza nyumba sita, kabla ya kuwateka nyara vijana watano ambao, hata hivyo, baadaye walifanikiwa kuponyoka mikononi mwao na kurejea nyumbani. 

Kulingana na idara ya polisi ya Kenya, hatua ya vikosi vya jeshi la Ethiopia vinakiuka mkataba wa mipaka baina ya mataifa hayo mawili. Akizungumza akiwa mjini Sololo, kamanda wa polisi jimboni Marsabit, Steve Oloo, amesema hatua hiyo ya vikosi vya jeshi la polisi vya Ethiopia kuingia nchini bila idhini na kufanya mashambulizi kwa raia wasiokuwa na hatia haikuwa sahihi na wala haikubaliki.

"Tungeomba tuheshimiwe kama kenya,na kama kuna jambo ambalo watu wa Ethiopia wanaona si nzuri,basi wafuate utaratibu ili tukae na amani na jirani. Hawa watu wote ni majirani,kuna wanaokaa hapa na wanafanya biashara zao kule Ethiopia," alisema Oloo.

Äthiopien Lebensmittellieferung in Moyale (DW/M. Kwena)

Wakaazi wa Wayye Goda, Marsabit wakipokea chakula cha msaada

Kamanda huyo wa polisi amesema kuwa vitengo tofauti vya polisi vitakuwa vinashika doria eneo hilo la mpakani huku akiwataka wakaazi waliotoroka makwao kurejea kwa hiari.

Kulingana na wanakijiji, wanajeshi wa Ethiopia waliingia kijiji humo na kuanza kuwapiga watu waliokuwa wamejificha majumbani mwao kabla yao kuondoka na vijana watano, kama anaavyoeleza mkaazi mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaka kutaja jina lake.

"Wanajeshi wa Ethiopia walipokuja kwetu, tuliingiwa na hofu kwa sababu walikuwa na silaha na wengine wakatoroka na wengine wetu tukajifungia ndani ya nyumba zetu. Wanajeshi hao kisha waliwateka watoto wakidai ni shifta. Kwa ujumla, waliondoka na watu watano."

Kulingana na serikali ya Kenya, hali inayoshuhudiwa kwa sasa itadhibitiwa na kamati za usalama kwenye mpaka huo. Akizungumza na DW kwa njia ya simu, msemaji wa serikali ya Kenya, Cyrus Oguna, amesema kuwa ukosefu wa usalama kwenye mpaka huo mara nyingi huchangiwa na wizi wa mifugo:

"Kuna kamati husika kutoka pande zote mbili na kazi ya kamati hiyo ni kutatua matatizo ambayo huenda yakaharibu usalama wa mpakani. Kwa hivyo, hakuna kitu kinachohitaji Umoja wa Mataifa kuingilia kati kwa kuwa si jambo ambalo limeshinda kamati hiyo kutatua," alisisitiza Oguna

Msimamo huo wa Bwana Oguna unafuatia kilio cha wakaazi cha kuutaka Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuingilia kati ili kupata suluhisho la mizozo ya mara kwa mara ambayo inazidisha uhasama kati ya wakaazi wanaoishi mpakani na wenzao wa Ethiopia.