Wahariri wajadili tangazo la Merkel | Magazetini | DW | 22.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Wahariri wajadili tangazo la Merkel

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani (22.03.2018) wamejishughulisha na tangazo la serikali la kansela Angela Merkel, kashfa ya data ya Facebook na muungano kati ya kampuni ya dawa ya Ujerumani Bayer na Monsanto.

Bundestag - Angela Merkel gibt Regierungserklärung ab (Getty Images/AFP/T. Schwarz)

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel

Gazeti la Frankfurt Allgemeine linaandika: Katika tangazo lake la kwanza la serikali kansela Merkel alizungumzia masuala ya ndani na nje yaliyotakiwa kugusiwa kupitia fursa hiyo. Mada moja lakini ndiyo iliyokuwa na uzito mkubwa kupita zote ambayo ilitawala mijadala katika awamu iliyopita ya utawala wa Merkel na ambayo Ujerumani itachukua miongo kadhaa kuishughulikia: Uhamiaji, utangamano, kuwajumuisha wageni katika jamii na mshikamano.

Mhariri anasema Merkel analazimika kuutetea mustakabali wake kwani mpasuko wa kisiasa uliopo nchini haujasababishwa tu na sera yake kuhusu wakimbizi, ingawa suala hili lililigawa taifa. Kansela amezungumzia fahari ya Ujerumani, lakini kwa upande mwingine kuna ukosoaji kutokana na serikali kushindwa kutafuta ufumbuzi.

Gazeti la Mannheimer Morgen linasema sio tu Horst Seehofer anayempa changamoto kansela Merkel, bali pia mkosoaji wake mkubwa, Jens Sphan. Mhariri anasema bila shaka kibarua cha kuitawala Ujerumani kimekuwa kigumu. Hata hivyo kutokana na uzoefu, Merkel kila mara amekuwa kiongozi mwenye nguvu anapokabiliwa na changamoto kubwa.

Kashfa data inayoikabili Facebook

Mada ya pili inahusu kashfa ya data inayoikabili kampuni ya Facebook. Gazeti la Hannoversche Allgemeine linaandika: Ni kashfa ambayo ni zaidi ya kuvuja kwa data. Ni kashfa inayohusu kubadilika kwa hali halisi ya kisiasa: Hisia ambazo zilifanya kupikwa kutumia mashine kutumia data za watumiaji wa mtandao wa Facebook. Haya yote kwa upande mmoja hayakubaliki, lakini mtu anaweza kusema hayajafikia kiwango cha kuitwa mashambulizi dhidi ya demorasia.

Naye mhariri wa gazeti la Rhein-Necker la mjini Heidelberg kuhusu kashfa ya Facebook anasema ni suala la kukisia kwamba kampuni ya Cambridge Analytica inakwenda mbali mno kiasi cha kuvuka mipaka katika kutafuta ufanisi. Hata hivyo kashfa hii inaleta jambo zuri: watu wanaanza kuhoji kuhusu Facebook ni nini hasa: Biashara inayotumia data zao. Pengine kashfa hii itaifanya Facebook isiendelee kukua.

Kampuni ya Bayer na Monsanto kuungana

Wahariri pia wamezungumzia kuungana kwa kampuni ya dawa ya Bayer na Monsanto. Gazeti la Tagesspiegel la mjini Berlin linasema kwa wakosoaji, mpango wa kampuni ya Bayer na Monsanto kuungana si harusi inayofanyika mbinguni, bali ni ndoa inayofanyika jehanamu.

Kwa mujibu wa sheria uamuzi wa makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels kukubali ni ya haki. Ujerumani kama kituo cha uvumbuzi inatakiwa kunufaika iwapo kuungana kwa makampuni haya makubwa kutazaa matunda kwa kampuni ya Bayer katika kipindi kirefu kijacho. Mhariri anamalizia kw akusema kampuni inatakiwa kuwajibu wakosoaji wake, vinginevyo  mbegu hazitaota.

Uislamu ni sehemu ya Ujerumani

Mada nyingine iliyoangaziwa katika magazeti ya Ujerumani hii leo ni suala la Uislamu. Mhariri wa gazeti la Emder anauliza je, Uislamu ni sehemu ya Ujerumani? Mhariri anatilia maanani kwamba suala hili liliwahi kuibuliwa na rais wa zamani wa shirikisho la Ujerumani Christian Wulff. Katika msimamo wake alisema mnamo mwaka 2010 kwamba uislamu ni shemeu ya Ujerumani.

Kwa sasa hisia zimebadilika humu nchini. Ni wachache wanaozungumzia mpasuko katika jamii. Bila shaka serikali mpya ya mseto inakabiliwa na mpasuko, hususan kati ya vyama ndugu ya Christian Democratic Union, CDU na Christian Social Union, CSU. Kansela Merkel halizungumzii suala hilo, badala yake anarudia suala la uislamu na kulipa uzito ionekana kana kwamba sasa uislamu umekuwa sehemu ya Ujerumani. Hakuna jipya!

Mwandishi: Josephat Charo/Inlandspresse

Mhariri:Saumu Mwasimba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com